Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi adai kigogo wa zamani Rahco hakuzingatia manunuzi

Mon, 20 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Reginald Malele, shahidi  wa kwanza katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wa Kampuni Hodhi ya Mali za Shirika la Reli (Rahco)  ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa alimshauri aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo, Benhardard Tito kuhusu manunuzi yasiyozingatia taratibu.

Shahidi huyo ameeleza hayo leo Jumatatu Mei 20, 2019 wakati akiongozwa na wakili wa  Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Maghela Ndimbo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Malele ambaye ni kaimu mkurugenzi wa manunuzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), amesema Agosti 18, 2015 alipewa maelekezo na Tito kuandika  barua za ahadi ya mkutano kwenda kwa mwenyekiti wa bodi ya zabuni, Ibrahim Kipalo kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi reli ya kisasa.

Malele amedai alimshauri kwamba sheria ya manunuzi na kanuni zake (PPA) hazitambui suala la ahadi ya mkutano huo na kwamba manunuzi yoyote yatakayofanyika bila bodi ya zabuni  kuthibitisha, si sahihi.

Ameeleza kuwa alishauri mamlaka ya manunuzi ipewe taarifa ndani ya siku 14 kuhusu zabuni mpya kabla ya kutangazwa na kwamba kila kitengo cha manunuzi kina nafasi yake katika utekelezaji wa mradi wa reli ya kisasa (SGR).

Malele aliendelea kudai baada ya kutoa ushauri huo, Agosti 19, 2015 Tito alimjibu kwamba tayari Serikali imeidhinisha Dola za Marekani 1,959,516.44 kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa yenye urefu wa kilometa mbili.

Pia Soma

Amesema ujenzi huo ungefanywa na Kampuni ya M/S China Railway Construction Corporation eneo la Soga na ulitakiwa kuanza mapema iwezekanavyo.

Amedai  kuwa baada ya kumueleza alijibu  ujenzi wa SGR hiyo utagharimu Sh2,154,212,000 fedha ambazo zilithibitishwa na Serikali na wameelekeza kazi kuanza mara moja.

Shahidi huyo amesema, “Kwa maelekezo aliyopewa maana yake hakuzingatia maelekezo yangu hivyo baada ya hapo nilimpelekea barua mkurugenzi kwa ajili ya kutia sahihi lakini utaratibu wa manunuzi haukuzingatiwa.”

Katika ushahidi wake Malele aliendelea kudai kwamba walienda kuomba kibali cha bodi ya zabuni ili kuanza mchakato wa kuthibitisha manunuzi ambayo yalitakiwa kufanyika kwa njia ya ushindani na baada ya kupitia nyaraka waligundua utekelezaji wa mradi huo ulianza kutekelezwa bila kibali cha bodi ya wazabuni.

Katika kesi hiyo mbali na Tito, washtakiwa wengine ni Mwanasheria wa Rahco, Emmanuel Massawe na mfanyabiashara ambaye pia ni mwakilishi wa kampuni ya Rothschild (South Africa) Proprietary Limited, Kanji Mwinyijuma.

Katika kesi ya msingi, washitakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka nane ikiwamo uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya madaraka, kula njama na kuisababishia kampuni ya Rahco hasara ya dola za Marekani 527,540.

Chanzo: mwananchi.co.tz