Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi adai hajui katiba ya Chadema, kesi ya kina Mdee

Chaema 19 Kortin Mdee .jpeg Shahidi adai hajui katiba ya Chadema, kesi ya kina Mdee

Fri, 8 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Aliyekuwa mbunge wa Chadema na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema, Maulida Anna Komu ameieleza Mahakama haifahamu vizuri katiba ya chama chake kwa sababu hana uzoefu wa kuisoma.

Komu (73) alieleza hayo, jana katika Mahakama Kuu Masijala Kuu, Dar es Salaam, wakati akitoa ushahidi wake katika kesi ya kikatiba, kupinga wabunge 19 wa viti maalumu wa Chadema akiwemo Halima Mdee kuvuliwa uanachama. Mdee ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) na wenzake 18 walifungua shauri hilo Mahakama Kuu Masjala Kuu ya Dar es Salaam, wakipinga kufukuzwa uanachama kwa utaratibu wa Mapitio ya Mahakama.

Kuhojiwa kwa bodi ya wadhamini ya Chadema kunatokana na maombi waliyowasilisha mahakamani hapo, baada ya kupokea kiapo kinzani cha maombi namba moja (bodi ya wadhamini ya Chadema) kuitwa kwa ajili ya kujibu.

Akihojiwa maswali ya dodoso ya wakili wa waleta maombi, Ipilinga Panya akishirikiana na Aliko Mwamanenge na Edson Kilatu, mbele ya Jaji Syprian Mkeha, shahidi huyo alidai taarifa zote zinazohusiana na chama hicho huzipata kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika na sio kwa mtu mwingine kwa sababu huwa hashiriki vikao vya Kamati Kuu wala Baraza Kuu.

"Hata taarifa ya wabunge 19 wa Viti Maalumu Chadema, kutofika kwenye Kamati Kuu ya chama hicho kwa ajili ya kuhojiwa kwa kuhofia usalama wao, nilipewa na chama changu kupitia Katibu Mkuu" alisema Komu.

Alidai Chadema iliwaandikia barua wabunge hao 19, ikiwataka wajieleza mbele ya Kamati Kuu ya chama hicho, baada ya kuwatuhumu kuwa wameenda Dodoma kuapishwa na kuwa wabunge, kinyume cha sheria.

"Baada ya Chadema kuwaita waleta maombi hao (wabunge 19 vya viti Maalumu) kwenda kujieleza mbele ya kamati Kuu, hawakwenda na walisema ulinzi ulikuwa mdogo ndio maana hawakufanya hivyo," alisema

Komu ambaye aliingia mahakamani akiwa na mkongojo na baada ya muda aliomuomba Jaji asimame kidogo kwa kuwa mguu wake ulikuwa unauma, alisema alijiunga na Chadema mwaka 1992 na kushika nafasi ya makamu Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini wa chama hicho.

Alipoulizwa alitoa wapi taarifa kuhusu kina Halima Mdee na wenzake kughushi barua kutoka Tume ya Taifa Uchaguzi zinazoonyesha kuteuliwa kwenda kuapishwa, alidai kuwa alisoma kwenye kiapo kinzani.

Jaji Mkeha aliahirisha kesi hiyo hadi leo itakapoendelea kwa mjumbe wa Bodi ya Udhamini wa Chadema, Francis Mushi kuhojiwa na upande wa waleta maombi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live