Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi adai Sabaya Kumtishia maisha

Ce5ae28b98f4eaccddba1b009707564c.jpeg Aliekuwa mkuu wa wilaya Hai, Ole Sabaya

Fri, 6 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SHAHIDI wa saba katika kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya (34) na wenzake wawili, amedai mahakamani kuwa, uchunguzi wa awali uligundua wananchi wawili, Hajirini Al Saad na Norma Jasin walipigwa, kuporwa na kutishiwa kwa silaha.

Shahidi huo ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arusha, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Gwakisa Minga alidai jana kuwa, baada ya kubaini hayo alitoa taarifa kwa viongozi wake wa juu akiwemo Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), Mchunguzi na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa, Mwalufambo ambao walimwelekeza amjulishe Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kenani Kihongosi.

Minga alieleza hayo wakati akiongozwa na Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavula mbele ya Hakimu Mwandamizi, Odira Amworo.

Alidai saa 6 usiku Mkuu wa Polisi Wilaya alimpigia simu arudi kituo kikuu cha polisi na alifanya hivyo.

Alidai alipofika kituoni hapo alimkuta Diwani wa Kata ya Sombetini jijini Arusha, Bakari Msangi akiwa na mkewe na baada ya kumwangalia usoni aliona kila dalili ya kupigwa kwa kuwa uso ulikuwa mwekundu na masikioni kulikuwa kukitoka damu.

Alidai baada ya kutoa maelezo, Msangi alipewa fomu ya matibabu ya kipolisi (PF3) kwenda katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kwa ajili ya matibabu.

Alidai alimweleza Sabaya kuwa watuhumiwa wake hawana kesi ya jinai hivyo polisi iliwaachia.

Minga aliendelea kudai kuwa, Sabaya alimwamuru msaidizi wake, Silvester Nyengu aende katika gari achukue simu za Hajirini na Norma ili wakabidhiwe na kwamba hilo lilifanyika ofisini kwake.

Kwa mujibu wa Minga, walijiridhisha kuwa Sabaya na vijana wake walitenda makosa lakini walishindwa kumkamata kwa kuwa alikuwa mteule wa Rais.

Alidai waliendelea na utaratibu mwingine wa kipelelezi wa kesi hiyo na baada ya kuzingatia taratibu za kiserikali, Sabaya alikamatwa, akaandika maelezo na kushitakiwa.

Chavula aliiomba Mahakama fomu ya PF3 iwe kielelezo katika kesi hiyo na mawakili wa utetezi hawakuwa na pingamizi na kielelezo hicho kilikuwa P1 na mawakili wa utetezi hawakutaka daktari aliyejaza fomu hiyo kuwa mmoja wa mashahidi kwa kuwa fomu hiyo ilikuwa ikijieleza vizuri na upande wa Jamhuri uliridhia.

Alidai katika maelezo yake, Msangi alidai kupekuliwa na kuporwa Sh 390,000 na alipigwa na kutekwa na kuzungushwa maeneo ya jiji Arusha kabla ya kuachiwa na Sabaya na wenzake na baada ya kuachiwa alitoa taarifa kwa OCD wa Arusha.

Minga alidai kikosi kazi cha ukachero kilianza kazi na kwenda dukani Shahiid Store na Norman alifungua duka hilo na kukuta likiwa limevurugwa, kamera za CCTV nne zilichezewa kwa lengo la kutoonesha tukio na aliona damu na maji maji chini.

Alisema yeye ni Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Wilaya ya Arusha na hakuna kosa la jinai ambalo litafanyika katika wilaya hiyo bila yeye kujua.

Chanzo: www.habarileo.co.tz