Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi adai Gugai alisaini nyaraka bila kufuata utaratibu

93532 Pic+gugai Shahidi adai Gugai alisaini nyaraka bila kufuata utaratibu

Wed, 29 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mlezi Makuka, mkuu wa ofisi ya kanda ya mashariki bodi ya usajili wa ubunifu majengo (AQRDB) ameieleza mahakama kuwa anatambua aliyekuwa mhasibu mkuu wa Takukuru, Godfrey Gugai alisaini nyaraka za miradi miwili kinyume na utaratibu wa bodi ya usajili wa majengo.

Makuka ambaye ni shahidi wa 29 katika kesi ya utakatishaji fedha na kumiliki mali zisizolingana na kipato chake inayomkabili Gugai ameeleza hayo leo Jumanne Januari 28, 2020 katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 382 ya mwaka 2017, Gugai na mwenzake watatu wanakabiliwa na makosa 43 ikiwemo ya kughushi, utakatishaji fedha na kumiliki mali zilizozidi kipato halali linalomkabili Gugai.

Akiongozwa na wakili wa Serikali mwandamizi, Awamu Mbagwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba shahidi huyo amedai miradi miwili iliyosainiwa na Gugai ilikiuka utaratibu wa bodi ya usajili wa majengo kwa mujibu wa taratibu za usajili.

"Namfahamu Gugai kama mwendelezaji wa miradi ambayo imesajiliwa katika bodi baada ya kupitia nyaraka zinazohusiana na jina hilo na kupata miradi miwili ambayo baada ya kuzipata nyaraka hizo nilihojiwa na Takukuru na kisha kuziandaa na kuzikabidhi kwa  ofisa huyo.”

"Fomu zinatakiwa kutolewa na mtaalamu wa majengo kutoka bodi ya wahandisi na kusainiwa na kampuni husika ya ujenzi,” amedai Makuka.

Pia Soma

Advertisement
Amedai nyaraka za miradi hiyo ni pamoja na mkataba wa ujenzi wa makazi ya kuishi wenye namba 34 na 35 ambayo kila mmoja una vielelezo vitatu  vya usajili pamoja na michoro ya ramani na mikataba ya mradi  uliopo Bunju na Ununio.

Shahidi huyo aliwasilisha kielelezo namba 34 mahakamani hapo ambacho ni fomu husika yenye jina la mwendelezaji miradi huo ambaye ni Gugai ikionyesha kiwanja husika namba 64 kilichopo Ununio Wilaya ya Kinondoni chenye mchoro wa nyumba nne za biashara zenye ghorofa moja zilizojengwa kwa Sh540 milioni.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 3, 4 na 5, 2020.

Tayari mashahidi 28 wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya Gugai.

Mbali na Gugai washtakiwa wengine ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.

Katika kesi ya msingi, Gugai na mwenzake, wanakabiliwa na makosa 43, kati ya hayo 19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali, ambalo linamkabili Gugai.

Gugai anakabiliwa na kosa la kumiliki mali kinyume na kipato chake akidaiwa kutenda kosa hilo kati ya Januari 2005 na Desemba 2015.

Inadaiwa kuwa akiwa Takukuru, Dar es Salaam, alikuwa akimiliki mali za zaidi ya Sh3.6 bilioni zisizolingana na kipato chake huku akishindwa kuzitolea maelezo.

Chanzo: mwananchi.co.tz