Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi aangua mahakamani kilio akimtambua mtuhumiwa wa mauaji wa mumewe

Mahakama Mahakama Shahidi aangua mahakamani kilio akimtambua mtuhumiwa wa mauaji wa mumewe

Tue, 14 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza iliyoketi Geita, jana iliahirishwa mahakama kwa muda baada ya kusikiliza ushahidi uliotolewa na mke wa marehemu, Samwel Songoma, aliyeuawa kwa kupigwa risasi na majambazi waliopora fedha zake.

Shahidi huyo ambaye ni wa nne kwa upande wa mashtaka, alitolewa nje ya mahakama kwa muda baada ya kuangua kilio alipotakiwa kumtambua mtu aliyemuua mume wake.

Mshtakiwa katika kesi hiyo ni Daniani Adrea, maarufu Kamkono.

Mshtakiwa huyo alipandishwa kizimbani mbele ya Jaji Lilian Itemba na aliposomewa shtaka lake alikana kuhusika na kosa la mauaji ya Samwel Songoma kwa kumpiga risasi tumboni.

Upande wa Jamhuri ulikuwa ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Janeth Kisibo, ambaye alisema atakuwa na mashahidi watatu na yuko tayari kuwasikiliza.

Jaji Itemba alimuuliza wakili wa kujitegemea Penina Mashimba, anayemtetea mshtakiwa huyo kama yuko tayari kusikiliza mashahidi watatu wa upande wa Jamhuri na kujibu yuko tayari.

Shahidi wanne wa upande wa Jamhuri, Elena Hemillana (46), ambaye ni mke wa marehemu, akiongozwa na Wakili wa Serikali Janeth Kisibo, alidai kuwa mwaka 2011 alikuwa anaishi katika Kijiji cha Lyobaika, Wilaya ya Bukombe na mume wake Samwel Songoma, ambaye kwa sasa ni marehemu aliyekuwa akifanya kazi ya kuuza madini.

Hemillana alidai Julai 2, mwaka 2013, majira ya usiku alikuwa nyumbani kwake wakiwa wamelala na mume wake na kuvamiwa na majambazi yaliyovunja mlango na kuingia ndani. Alidai kuwa majambazi hao waliomba fedha kwa mume wake na aliwapatia hizo, hata hivyo, hakuweza kujua jumla ya kiasi alichowapa.

Aliendelea kudai kuwa baada ya kuwapatia fedha hizo, majambazi hao walimwambia mume wake aongeze fedha, lakini aliwajibu kuwa hana zingine ndipo walipompiga risasi tumboni na kuanguka chini na kufariki dunia.

Shahidi huyo alidai kuwa majambazi hao waliingia chumbani na kuanza kutafuta fedha kwa kupekua vitu mbalimbali na kwamba wakati wakipekua alifanikiwa kumtambua mmoja wa majambazi hao.

Alimtaja kwa jina maarufu la Kamkono kwa sababu alikuwa fundi ujenzi katika kijiji hicho.

Alipotakiwa na Wakili wa Serikali akaonyeshe mtu aliyemfahamu wakati wa tukio mahakamani hapo, shahidi huyo alimgusa bega mshtakiwa huyo na kuangua kilio akisema; “Ee Mungu wangu nisaidie, ee Mungu wangu nitie nguvu”.

Shahidi huyo alitolewa nje ya mahakama huku akiangua kilio na baada ya nusu saa alirudishwa kizimbani na kuendelea kutoa ushahidi wake.

Mahojiano kati ya wakili na shahidi yaliendelea kama ifuatavyo:

Wakili: Utaratibu ulifanyika wa gwaride la utambuzi?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Ganda la risasi liliokotwa wapi?

Shahidi: Nje.

Baada ya mahojiano hayo, wakili wa serikali aliomba mahakama hiyo iahirishe kesi hiyo hadi muda wa saa tisa jioni (jana).

Jaji Itemba alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi muda huo.

Awali, akisoma hati ya mashtaka, Karani wa mahakama hiyo Paschal Alphonce, alidai kuwa Julai 2, mwaka 2013, majira ya usiku katika Kijiji cha Lyobaika, Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita, mshtakiwa alimuua Samwel Songoma kwa kumpiga risasi tumboni na kufariki dunia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live