Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sh3 milioni za mauzo ya tikiti zasababisha mauaji Geita

49092 Tikiti+pic.png

Thu, 28 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbogwe. Neema ya mauzo ya Sh3 milioni yaliyotokana na kilimo cha zao la tikitimaji yametumbukia nyongo familia ya mkulima wa Kijiji cha Nyag’holongo, Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita baada ya watu wanaosadikiwa ni majambazi kuvamia na kumuua baba wa familia hiyo.

Tukio hilo lilitokea saa 7:00 usiku wa kuamkia juzi baada ya watu hao kumchoma kwa vitu vyenye ncha kali baba huyo, Fikiri Kazyoba (49), wakimshinikiza kuwapa fedha za mauzo ya tikitimaji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi na msako dhidi ya watuhumiwa na amewataka raia wema wenye taarifa zitakazosaidia wahusika kutiwa mbaroni kujitokeza.

Akizungumzia tukio hilo, ofisa mtendaji wa Kata ya Nanda, Alizinus Mtalemwa alisema kabla ya kuvamiwa usiku, mchana wa siku ya tukio, Kazyoba alienda mnadani kwa lengo la kununua mifugo lakini alikosa na kurejea nyumbani.

“Usiku ulipofika ndipo kundi la watu wanaosadikiwa kuwa majambazi lilipovamia familia hiyo na kuanza kumchoma Kazyoba na vitu vyenye ncha kali wakimshinikiza awape fedha za mauzo ya tikitimaji alizouza siku chache zilizopita,” alisema Mtalemwa.

Mtendaji huyo wa kata aliwaomba wananchi wanapouza mifugo na mazao yao kuweka fedha zao benki badala ya kuzihifadhi nyumbani kuepuka vitendo vya wizi.



Chanzo: mwananchi.co.tz