Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Seth: Sijaonana na wakili wangu kwa miezi sita

59286 Sethpic

Thu, 23 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mfanyabiashara Harbinder Seth anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuonana na wakili wake gerezani kwa maelezo kuwa hawajaonana kwa kipindi cha miezi sita.

Seth na mwezake James Rugemalira wanaokabiliwa na mashtaka 12 yakiwemo ya utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27 kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani hapo Juni 19, 2017. 

Seth amedai hayo  leo Alhamisi Mei 23, 2019 baada ya wakili wa Serikali, Wankyo Simon kudai  mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika.

Baada ya maelezo hayo,  Seth alinyoosha mkono na kudai wakili wake anapokwenda gerezani ili kuchukua   maelekezo anayotaka kumpa,  maofisa wa Gereza wamekuwa wakimzuia kuonana naye.

"Naiomba mahakama imruhusu wakili wangu aje gerezani ili nionane naye  nataka nimpe maelekezo ya kesi yangu sasa ni miezi sita sijaonana naye," amedai Seth.

Hakimu Shahidi aliwataka maofisa wa Magereza kumruhusu Seth kuonana na wakili wake kwa kuwa anayo haki ya kufanya hivyo.

Pia Soma

Baada ya maelezo hayo hakimu Shahidi ameahirisha shauri hilo hadi Juni10, 2019 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Seth na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi, ikiwamo ya kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi nyaraka, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu,  kutakatisha fedha  na kuisababisha Serikali hasara ya dola za Marekani  22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

 

Washitakiwa hao wanadaiwa kuwa, Oktoba 18, 2011 na Machi 19 , 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ili kutenda kosa.

 

Aidha, inadaiwa katika shitaka la kujipatia fedha kwamba  kati ya  Novemba 28 na 29, 2011 na Januari 23,2014 katika makao makuu ya Benki ya Stanbic Kinondoni  na Benki ya Mkombozi tawi la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam  kwa ulaghai walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) dola za Marekani  22,198,544.60 na Sh 309, 461,300,158.27. 

 

Pia washitakiwa wote wanadaiwa kuisababishia Serikali hasara ambapo inadaiwa walitenda makosa hayo Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la  Kinondoni na kwa vitendo vyao waliisababishia Serikali hasara ya dola za Marekani 22, 198, 544.60 na Sh. 309,461,300,158.27.

 

Inadaiwa kati ya Novemba 29,2013 na Januari 23, 2014 maeneo tofauti Dar es Salaam kwa pamoja walitenda kosa la kutakatisha fedha kwa kuchukua fedha kutoka BoT ambazo ni dola za Marekani milioni 22.1 na Sh 309.4 bilioni wakati wakijua fedha hizo ni zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

 

Washitakiwa hao wapo rumande kwa kuwa mashitaka hayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz