Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yawaonya Polisi wanaokula rushwa

Askari Pic Data Serikali yawaonya Polisi wanaokula rushwa

Tue, 8 Feb 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Serikali imeaonya askari Polisi wa kanda maalum ya Tarime/Rorya wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa ili kuwalinda wanaojihusisha na vitendo vya ukeketaji wilayani Tarime

Akifungua kongamano la wadau wakati wa kilele cha Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukeketaji mjini hapa, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju amesema tayari anayo majina ya askari hao wanaodaiwa kula rushwa na siku zao zinahesabika.

"Haiwezekani Serikali ikatumia fedha nyingi kuanzisha Kanda maalumu ili idhibiti uharibifu na uhalifu halafu baadhi ya askari wanatumika kutoa taarifa pale ambapo RPC anapanga kwenda kuwakamata kisha watuhumiwa wanatoroka" amesema.

Akitoa taarifa ya hali ya ukeketaji, mkuu wa dawati la kijinsia kutoka Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Tarime/Rorya, Cloud Mtweve amesema kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita jumla ya matukio 15 ya ukeketaji yaliripotiwa polisi na watu 19 kukamatwa.

Amesema kuwa katika kipindi hicho jeshi hilo lilifungua mashauri matano mahakamani ambapo mashauri mawili yaliisha kwa mafanikio huku majalada mengine mawili yakiwa hatua za mwisho katika ofisi ya mwendesha mashtaka wa serikali kwa ajili ya maandalizi ya kupelekwa mahakamani.

Amesema kuwa zipo changamoto kadhaa ambazo jeshi hilo linakumbana nazo katika kupambana na ukeketeji ikiwemo suala la ukeketaji jumuishi baina ya Watanzania na Wakenya kutokana na mila ya ukeketaji kutekelezwa kwa wakazi wa upande wa Tanzania na ule wa Kenya.

Advertisement Kufuatia hali hiyo amesema kuwa tayari wameunda kikosi kazi cha pamoja chenye watu wanane kutoka kila upande ambapo wenyeviti wa kamati hiyo ni Wakuu wa Wilaya za Tarime nchini Tanzania na Mkuu wa Kilaya ya Kurya nchini Kenya ili kwa pamoja waweze kushirikiana kutokomeza vitendo hivyo.

"Ukeketaji ni 'organized crime ' yaani tulibaini kuwa sisi huku tukiwa na msako basi watu wa huku wanakubaliana na wenzao wa kule kwenda kufanyia ukeketaji upande wa pili kwa sababu mila zao zinaingiliana hivyo hivyo wakati wa msako kule wanakubalina kuja kufanyia huku kwa hiyo hiki kikosi kazi kitafanya kazi kwa pamoja" amesema.

Naye Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima ameitaka jamii kubadilika na kuachana na mila zilizopitwa na wakati.

"Mila zingine tunatakiwa kuzipima sio kila tulichorithi kinafaa, madhara ya ukeketaji ni mengi na makubwa ikiwemo maambukizi ya magonjwa kama ukimwi na pia ukeketaji unasababisha vifo hebu tubadilike" amesema Dk.Gwajima

Chanzo: www.mwananchi.co.tz