Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yasubiri ripoti kukamilisha upelelezi kesi ya Muharami

Muhami Kesi Serikali yasubiri ripoti kukamilisha upelelezi kesi ya Muharami

Wed, 2 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali inasubiri ripoti mbili kutoka katika kampuni mbili za simu ili kukamilisha upelelezi katika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine kilo 34.89 inayomkabili aliyekuwa kocha wa makipa wa timu ya Simba Sport Club, Muharami Sultan (40) na wenzake watano, iweze kuendelea na hatua nyingine.

Sultani na wenzake, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 71/2022 yenye mashtaka mawili ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilo 34.89.

Wakili wa Serikali, Erick Kamala ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu, leo Agosti 2, 2023 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

"Mheshimiwa hakimu, kesi hii imekuja kwa ajili ya kutajwa, kuna ripoti mbili kutoka Kampuni mbili za simu ambazo bado hazijawasilishwa kwetu, hivyo kutokana na Hali hii, tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa" amedai Kamala.

Wakili Kamala baada ya kueleza hayo, wakili wa washtakiwa hao Said Mzeri, ameutaka upande wa mashtaka kukamilisha haraka upelelezi kwa sababu hiyo sio mara ya kwanza kudai kuwa wanasubiri vielelezo.

"Mheshimiwa hakimu, naomba upande wa mashtaka wakamilishe kwa haraka upelelezi wao kwa kuwa kesi hii ni ya muda mrefu na hii sio mara ya kwanza kudai kuwa wanasubiri vielelezo kutoka kwenye hizo taasisi," amedai Mzeri.

Hakimu Mrio, baada ya kusikiliza hoja za pande zote, ameutaka upande wa mashtaka kuharakisha upelelele wa shauri hilo.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 18, 2023 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka linalowamkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Mbali na Sultani, washtakiwa wengine ni mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma, Kambi Zubery Seif; Said Matwiko mkazi Magole; Maulid Mzungu maarufu mbonde (54), mkazi wa kisemvule; John John maarufu ‘Chipanda’ (40) mkazi wa Kitunda na Sarah Joseph.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live