Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yashindwa kusoma maelezo ya awali kesi vigogo TRL

Tue, 30 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi inayowakabili vigogo 18 wa kampuni ya Reli Tanzania (TRL) umeshindwa kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao kutokana na kutokamilisha kuyaandaa.

Washtakiwa hao pamoja na aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Kipallo Kisamfu, wanakabiliwa na mashtaka 15 ya matumizi mabaya ya madaraka.

Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Moghela Ndimbo, aliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumanne Aprili 30, 2019 kuwa shauri hilo lililetwa kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao lakini hawajakamilisha kuyaandaa.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kelvin Mhina ameahirisha shauri hilo hadi Mei 27, 2019 kwa ajili ya kusoma maelezo ya awali na washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana.

Mbali na Kisamfu washtakiwa wengine ni Gilbert Minja, Paschal Mafikiri, Kaimu Mhandisi Mitambo Mkuu na Mathias Massae ambaye ni Kaimu Mhandisi Ujenzi Mkuu.

Wengine ni Anthony Munishi, Meneja Usambazaji; Charles Ndenge, Kaimu Meneja wa Usafirishaji; Ferdinand Soka, Kaimu Meneja Msaidizi wa Usambazaji; na Muungano Kaupunda, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ufundi.

Pia, wapo Joseph Syaizyagi, Kedmond Mapunda, Lowland Simtengu, Ngoso Joseph Ngosomwile, Yonah Shija, Malumbo Jadi Malumbo, Stephan Kavombwe, Donatus Bandebe, John Charles na Ally Mwangila.

Katika kesi hiyo, washtakiwa wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kuingia mikataba ya zabuni ya ununuzi wa vichwa vya treni na kuipa zabuni hiyo kampuni ya Hindusthan Engineering and Industries Limited.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Oktoba 23, 2012 na Aprili 26, 2015.



Chanzo: mwananchi.co.tz