Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yashinda kesi dhamana makosa ya jinai

1f1e066d6d222c9d0018f2f02dbba2ed Serikali yashinda kesi dhamana makosa ya jinai

Thu, 6 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAHAKAMA ya Rufaa Tanzania imetengua uamuzi wa Mahakama Kuu, ulioelekeza kuwa Kifungu cha 148 (5) cha Sheria ya Makosa ya Jinai, kinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kwa kufanya makosa yaliyoainishwa na kifungu hicho kutokuwa na dhamana.

Baadhi ya makosa katika kifungu hicho ni ya mauaji, unyang'anyi wa kutumia silaha, uhaini, ugaidi, utakatishaji fedha, na kesi za dawa za kulevya.

Makosa mengine ni mtu aliyewahi kufungwa miaka 30 jela hataweza kupata dhamana, mtu aliyepewa dhamana akashindwa kutekeleza masharti ya dhamana au akaruka dhamana, pale mtu anatakiwa kukaa ndani kwa ajili ya usalama wake au kama kosa linazidi Sh milioni 10.

Hukumu hiyo ilisomwa jijini Dar es Salaam jana na Naibu Msajili Mwandamizi wa mahakama hiyo, Eva Nkya mbele.

Alisema jopo la majaji watano Stella Mugasha, Gerald Ndika, Jacobs Mwambegele, Mwanaisha Kwariko na Ignas Kitusi, limeamua kwa pamoja kuwa Kifungu cha 148(5) A mpaka E kinachobainisha makosa ambayo hayadhaminiki, hakikinzani na Katiba ya Tanzania na kinakidhi masharti, hivyo masharti ya kutokuwa na dhamana kwa makosa hayo, yatabaki kama ilivyokuwa.

Alisema majaji hao watano kwa pamoja wameamua kuwa kifungu hicho kinachozuia dhamana hakikinzani na Katiba, hivyo masharti ya kutokuwa na dhamana kwa makosa hayo, yatabaki kama ilivyokuwa.

Kutokana na hali hiyo, jopo hilo limekubaliana na hoja za serikali katika rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wakipinga uamuzi wa Mahakama Kuu ulioruhusu dhamana kwa baadhi ya makosa ya jinai yasiyokuwa na dhamana.

Katika uamuzi uliotolewa Mei 18 mwaka huu, Mahakama Kuu ilieleza kuwa Kifungu cha 148 (5) cha Sheria ya Makosa ya Jinai kinakiuka Katiba ya Tanzania.

Mahakama hiyo ilitoa miezi 18 kwa Serikali kuhakikisha wanawasilisha muswada bungeni kubadilisha sheria hiyo.

Baada ya uamuzi huo, DPP na AG walikata rufaa namba 175/2020 wakipinga uamuzi wa Mahakama Kuu katika shauri namba 29/2019 lililofunguliwa na Dickson Sanga, aliyetaka makosa hayo yawe na dhamana kwa sababu kifungu kilichokuwa kinazuia dhamana,kinakiuka Katiba ya Tanzania.

Katika rufaa yake DPP na AG walidai kifungu hicho hakikiuki Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Walidai kwamba Mahakama Kuu ilikosea kisheria kutamka kuwa Kifungu namba 148 (5) kinakiuka Ibara ya 13 (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia walidai kuwa Mahakama hiyo ilifanya makosa ya kisheria kutamka kuwa kifungu hicho namba 148 cha Sheria ya Makosa ya Jinai hakithibitishwi na Ibara ya 15(1) na (2) (a ) ya Katiba wa Jamhuri ya Muungano, kwamba kifungu hicho kilikiuka Katiba pamoja na kwamba mjibu rufaa alishindwa kuthibitisha madai yake bila kuacha shaka.

Chanzo: habarileo.co.tz