Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yapinga dhamana anayedaiwa kusafirisha kobe

Kobe Pic Raia wa Ukraine, Orga Kryashtop (kushoto) akiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaa

Wed, 12 Jul 2023 Chanzo: Mwananchi

Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Tanzania (DPP) amewasilisha maombi ya kuzuia dhamana dhidi ya raia wa Ukraine, Orga Kryashtop baada ya mshtakiwa kudai kuruka dhamana katika kesi nyingine iliyofunguliwa nje ya nchi.

Kryshtop anakabiliwa na mashtaka mawili, likiwemo la kusafirisha kobe 116 wenye thamani ya Sh18.9 milioni bila kuwa na kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori nchini.

DPP aliwasilisha maombi hayo leo Julai 12, 2023 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Wakiwasilisha maombi hayo, Wakili wa Serikali, Elizabeth Mkunde akishirikiana na Judith Kyamba alieieleza Mahakama hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Amir Msumi, kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kwamba upande wa mashtaka umepeleka maombi ya kuzuia dhamana dhidi ya mshtakiwa huyo kutokana kuruka dhamana katika kesi nyingine aliyokuwa amefunguliwa nje ya nchi.

Alidai kuwa kutokana na mazingira hayo, Serikali imewasilisha kiapo cha Askari Polisi Obasi Valanguga Nguvila, ambapo pamoja na mambo mengine waliomba mahakama itumie kifungu cha 50 cha Sheria ya Makosa ya Jinai kikisomeka pamoja na kifungu cha 37 cha sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi kuondoa dhamana dhidi ya mshtakiwa huyo.

Mkunde amedai katika kiapo hicho, mshtakiwa kabla ya kuletwa katika Mahakama ya Kisutu na kufunguliwa kesi hiyo, alishafunguliwa kesi nyingine huko Thailand na baada ya kupewa dhamana, aliruka dhamana hiyo na kisha kutoroka.

Baada ya kuruka dhamana, mshtakiwa alikimbia, na kwamba askari wa Interpol wakishirikiana na vikosi vingine walifanikiwa kumkamata nchini Bulgaria na kisha kumleta Tanzania ambapo alifunguliwa kesi ya uhujumu uchumi namba 31/2023.

Amedai wakati anafunguliwa kesi hiyo upande wa mashtaka hawakuwa wanajua kama mshtakiwa alisharuka dhamana kwenye kesi nyingine, hivyo Mahakama ijielekeze katika vifungu hivyo.

Serikali baada ya kueleza hayo, Wakili wa mshtakiwa Faraji Ahmed, aliomba apewe muda ili nae awasilishe kiapo kinzani mahakamani hapo.

Hakimu Msumi baada ya kusikiliza maelekezo ya pande zote, alimtaka Wakili Ahmed kuwasilisha maombi yake kabla ya Julai 19, 2023 na kisha kuahirisha kesi hiyo hadi Julai 27, 2023 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande.

Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa alifikishwa mahakamani hapo Juni 19, 2023 na kusomea mashtaka yake.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa kati ya Januari Mosi hadi Julai 30, 2022 jijini Dar es Salaam, mshitakiwa alijihusisha na nyara za Serikali kwa kununua, kuuza na kusafirisha kobe 116 wenye thamani ya Sh 18,935,840 mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Shtaka la pili, inadaiwa katika tarehe hizo, eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA) uliopo wilaya ya Ilala, Kryshtop alikamatwa akiwa na kobe hao bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini.

Chanzo: Mwananchi