Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yamng’ang’ania Wang’anyi

Hukumu Pc Data Serikali yamng’ang’ania Wang’anyi

Sun, 18 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Kesi ya mfanyabiashara maarufu jijini Mwanza Jumanne Mahende Wang’anyi, ambayo iliamuriwa kusikilizwa upya baada ya hukumu ya kunyongwa kubatilishwa inaonekana kuwa ya moto kwa Serikali, iliyoamua kuiondoa mahakamani kisha kuifungua upya.

Mfanyabiashara huyo maarufu kama J4, anayemiliki kampuni ya mabasi ya J4 Express, alichiliwa huru juzi baada ya Serikali kuieleza Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kuwa haina nia ya kuendelea nayo, wakati upande wa mashtaka unaelekea kufunga ushahidi wake.

Wakili wa mfanyabiashara huyo, Peter Kibatala, alieleza jana kuwa muda mfupi tu baada ya mahakama kumwachia huru mteja wake kutokana na maombi ya Serikali, alikamatwa tena na maofisa wa Polisi waliompeleka Kituo Kikuu cha Polisi Mwanza.

Wakili Kibatala alisema jana Serikali ilimpandisha tena kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana na kumsomea upya mashtaka hayo ya mauaji katika kesi ya mauaji namba 20 ya mwaka 2022.

Hata hivyo, Kibatala alisema wameweka pingamizi wakidai kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kuendesha mwenendo wa kesi hiyo katika hatua hiyo kuiandaa kabla ya kuihamishia Mahakama Kuu itakakosikilizwa dhidi ya mshtakiwa kwa kuzingatia amri ya Mahakama Kuu ya kumwachia.

Wakili Kibatala alilieleza kuwa upande wa mashtaka ulilazimika kuiondoa kesi hiyo mahakamani baada ya mahakama hiyo kukataa kupokea vielelezo vyake vitatu vya ushahidi kwa nyakati tofauti, kufuatia mapingamizi aliyoyaweka kutokana na ukiukwaji wa matakwa ya kisheria.

“Hata hivyo jaji alisema kuwa ingawa amerekodi hoja zangu lakini hana cha kufanya, kwani sheria inamfunga mikono kwamba DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka) akishatoa taarifa hiyo chini ya kifungu hicho, basi kesi inaishia hapo. Hivyo aliamua kumwachilia huru ndipo wakamkamata tena.”

Awali mfanyabiashara huyo alihukumiwa na Mahakama Kuu adhabu ya kunyongwa mpaka kufa, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la mauaji ya watu wawili.

Alitiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu hiyo kwa kosa la kuwaua kwa makusudi Ally Abeid mkazi wa Igoma na Claudia Sikalwanda, mkazi wa Nyasaka Ilemela kwa kuwapiga risasi Julai 13, 2015 nje ya ofisi zake Nyakato Boma, wilayani Nyamagana jijini Mwanza.

Ingawa katika utetezi wake mfanyabiashara huyo alidai kuwa aliua bila kukusudia kwa kuwa alikuwa akijitetea baada ya kuvamiwa, lakini Jaji Sam Rumanyika aliukataa utetezi huo.

Chanzo: Mwananchi