Baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumfutia kesi ya uhujumu uchumi mfanyabiashara Jitesh Jayantilal Ladwa, Serikali imemkatia rufaa Mahakama Kuu ikitaka kesi hiyo irejeshwe.
Jitesh alipandishwa kizimbani kwa kesi ya uhujumu uchumi, akituhumiwa kughushi na kujihamishia hisa za wanahisa wenzake katika Kampuni ya Indian Ocean Hotels Limited, inayomiliki hoteli za Golden Tulip.
Hata hivyo, Mahakama ya Kisutu ilimfutia kesi hiyo baada ya kukubaliana na hoja za pingamizi za wakili wake, Jeremiah Mtobesya kuwa Mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya jinai.
Baada ya uamuzi huo, Serikali imekata rufaa Mahakama Kuu nayo ikiipinga Mahakama ya Kisutu kuwa haina mamlaka ya kutoa uamuzi kama huo wala kusikiliza pingamizi.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ester Martin alilieleza Mwananchi hivi karibuni kuwa Serikali imekata rufaa kupinga uamuzi mahakamani kumfutia mashtaka Jitesh huku ikiwa na sababu tatu.
Alidai kuwa bado wanasisitiza Mahakama ya Kisutu ilikosea kutoa uamuzi huo kwa kuwa haina mamlaka ya kuamua wala kusikiliza hoja yoyote kutoka kwa mshtakiwa.
Katika kesi hiyo, Jiteshi alikuwa akikabiliwa na mashtaka 24, yakiwamo ya kughushi, kujipatia hisa kwa udanganyifu na utakatishaji fedha.
Kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo kwa ajili ya uchunguzi wa awali kwa mujibu wa sheria, kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi yenye mamlaka ya kusikiliza na kuamua kesi za aina hiyo.
Baada ya kusomewa mashtaka, wakili Mtobesya anayemsimamia Jitesh alidai kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya jinai. Alidai kuwa kutokana na marekebisho ya Kifungu cha 4 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CAP), yaliyofanyika mwaka huu, Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya aina hiyo.
Wakili Mtobesya alisema katika marekebisho hayo kiliongezwa kifungu kidogo cha 3 kinachozuia kufunguliwa kwa shauri la jinai lenye masuala ya kimadai na kiutawala, mpaka kwanza masuala ya kimadai au ya kiutawala yatakapomalizika.