Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali ya Tanzania kutumia mashahidi 60, vielelezo 200 kesi vigogo wa Nida

91135 Pic+mashahidi Serikali ya Tanzania kutumia mashahidi 60, vielelezo 200 kesi vigogo wa Nida

Wed, 8 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mashahidi 60 wanatarajia kutoa ushahidi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) nchini Tanzania, Dickson Maimu na wenzake wanne.

Pia, vielelezo 200, vinatarajia kutolewa katika kesi hiyo, iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa kesi hiyo kukamilika na Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania ( DPP)  kuipa mamlaka, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 7/2019.

Maimu na wenzake wanne, wanakabiliwa na mashtaka 55 yakiwamo ya kutakatisha fedha na kuisababishia Serikali ya Tanzania hasara ya Sh1.175 bilioni.

Hayo yameelezwa jana Jumanne Januari 7, 2020 na wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladslaus Komanya akisaidiana na wakili wa Serikali Janeth Magoho, wakati akiwasomea hoja za awali(PH) washtakiwa hao.

Komanya aliwasomewa hoja za awali, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Salum Ally, wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa hao hoja za awali( PH).

“Mheshimiwa hakimu, upande wa mashtaka tunatarajia kuleta mashahidi 60 ambao watatoa ushahidi dhidi ya washtakiwa hawa, pia tutakuwa na vielelezo 200, ambavyo tutavitoa mahakamani hapa,” alidai Komanya.

Hata hivyo, washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yanayowakabili, walikubali majina yao lakini walikana mashtaka yanayowakabili.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Ally, aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 15, 2020, itakapoanza kusikilizwa ushahidi.

Mbali na Maimu, washtakiwa wengine  ni Ofisa Usafirishaji wa Nida, George Ntalima; Meneja Biashara wa Nida, Avelin Momburi;  Xavery Silverius maarufu kama Silverius Kayombo na mkurugenzi wa Sheria Nida, Sabina Raymond.

 

Kati ya mashtaka 55 waliosomewa washitakiwa hao, yapo ya  kuisababishia Serikali  hasara ya Sh1.175 bilioni; utakatishaji fedha; kughushi; kuwasilisha nyaraka za uongo ili kumdanganya mwajiri wao; kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu; matumizi mabaya ya madaraka na kuongoza genge la uhalifu.

Awali, washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka zaidi ya 20 lakini Januari 28, 2019 Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) aliwafutia mashtaka hayo, baada ya kueleza mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hiyo.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye, washtakiwa hao walifunguliwa kesi mpya ya uhujumu uchumi yenye mashtaka zaidi ya 50.

Chanzo: mwananchi.co.tz