Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sakata mtoto kubakwa: Polisi kutumia intelijensia

 ACP Pius Lutumo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo.

Tue, 21 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Siku mbili baada ya kuripotiwa tukio la kubakwa na kunyongwa binti wa miaka 10 kijijini Mipera, Kata ya Marui, wilayani Kisarawe, mkoani Pwani, huku zikipita siku tisa bila mtuhumiwa kukamatwa, Jeshi la Polisi limetuma intelijensia yake na kuwapa mashekhe jukumu zito.

Juzi, iliripotiwa tukio la mtoto (jina linahifadhiwa) mwanafunzi wa darasa la tatu, kufanyiwa ukatili huo na mtuhumiwa Ismail Mandanga, Kijiji cha Mianzi, ambaye sasa anawatishia wananchi na viongozi wa kijiji kwa panga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo, ambaye alipata taarifa za tukio hilo juzi kutoka kwa mwandishi wa habari hizi na kuahidi kufuatilia, alipotafutwa jana, alisema tayari ameshatuma intelijinsia yake.

“Baada ya taarifa nilifuatilia kwa OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) Kisarawe. Ni kweli tukio lipo limetokea siku za nyuma, lakini katika makosa kama haya huwa tunaangalia kosa kubwa na hapa ni la mauaji. Nimemwambia OCD asimamie mtuhumiwa akamatwe. Nategemea atakamatwa.

Kuhusu mtuhumiwa kutishia wananchi, Kamanda alisema alipoongea na OCD alithibitisha mtuhumiwa huyo kuonekana kwa kificho.

“Anaonekana kwa kificho, lakini tumetuma intelejensia katika maeneo hayo ndiyo maana nimesema tunategemea siku za karibuni tutamkamata,” alisema.

Alisema kwa sasa polisi wamesambazwa kwenye kata ambako kuna wakaguzi ambao moja ya maelekezo ni kufanya mikutano ya hadhara, kuongea na wananchi kuacha matendo hayo, wasihofu kutoa ushahidi au kutoa taarifa yoyote.

MAAGIZO MASHEHE

Shekhe wa Wilaya ya Kisarawe na Mwenyekiti Mwenza Kamati ya Amani na Mjumbe Kamati ya Maadili ya Mahakama, Ramadhan Kumbangulu, amesema pamoja na kulaani kitendo hicho ambacho hata vitabu vya dini vinakemea na kupinga, tayari wameshatoa maelekezo kwa mashehe.

“Uislamu unakataza mambo haya. Si jambo zuri. Nilipopata taarifa nilimpigia OCD Kisarawe kumweleza na viongozi wa dini hili jambo tumesema hatuwezi kukubali, tutalifuatilia mpaka mtuhumiwa akamatwe.

HALI ILIVYO

Shehe Kumbangulu amesema jiografia ya Kisarawe ni tofauti na sehemu nyingine, imekuwa ni ngumu kijiografia, mazingira ya kiuchumi ni duni na wakati mwingine matukio kama hayo yanapotokea inakuwa vigumu kusaidia, kutokana na watu wake kukosa elimu na woga.

Shekhe Kumbangulu anasema juhudi kubwa zinazofanyika ni kufanya makongamano na kutembelea kata kuelimisha jamii.

SMAJATA WAFUNGUKA

Suala la elimu limeungwa mkono pia na Mwenyekiti wa Kampeni Huru ya Kitaifa ya Kupinga Ukatili (SMAUJATA), Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania, Wilaya ya Kisarawe, Anectus Asingizibwe, akisema matukio hayo yamekuwa yakijitokeza wilayani humo na changamoto ikiwa ni uelewa mdogo wa watu namna ya kuripoti au kuzuia.

“Mtu anabakwa anakuja kutoa taarifa baada ya siku tatu, hata taratibu za kitabibu zikifanyika haziwezi kuona kitu. Mtu anabakwa, analawitiwa unamwogesha, ukija kumfikisha hospitalini kama ameoga huwezi kuona chochote.

“Mwisho wa siku watasema amebakwa, lakini ushahidi hakuna. Wananchi wanaishi maisha ya ujamaa sana na matukio haya yanapotokea mengi hufichwa.”

Asingizibwe anasema SMAUJATA ina miaka mitatu wilayani humo tangu mwaka 2022 wakielimisha wananchi na kueleza kuwa, Kiluvya imekuwa na matukio mengi ya ubakaji ambao unakosa ushahidi baada ya kupotea.

Amesema udhibiti wa matukio hayo ni mgumu kwa kuwa wananchi huogopa kutokana na ujirani mwema au kuhofia kuvunja undugu na huamua hukaa kimya.

“Kwa hiyo Wilaya ya Kisarawe na Pwani kwa ujumla imekuwa ikikatiliwa kwa namna hiyo. Kwa ujumla matukio mengi tunayafikisha mbele, lakini yanakosa ushahidi.”

JUHUDI ZINAZOFANYIKA

Ni kuhakikisha wanapata vibali vya halmashauri kwenda kwenye shule zote za msingi na sekondari.

Wamekutana na wanafunzi wa shule mbalimbali kuwaelimisha masuala ya ukatili, kufungua vilabu vya kupinga ukatili shuleni na kukutana na vyama vya walimu wilayani humo kupitia mikutano yao ya mwaka ya vyama vya walimu.

Kadhalika, amefanya mikutano na viongozi wa dini wilayani humo wanaoitwa Kamati ya Amani ya wilaya, ambayo Mwenyekiti wake ni Shekhe Mkuu wa wilaya na kushirikiana nao kufikisha elimu ya huduma ya msaada.

MWANANCHI JASIRI

Mariamu Kombe, Mwenyeji wa Marui Mwisho, anathibitisha kuwapo kwa uoga wa wananchi kutoa taarifa za matukio ya ukatili ingawa anasema, aina ya tukio hilo lilimfanya kujitoa kimasomaso.

“Nilipokea taarifa za tukio kutoka kwa mwanachi wa kijiji kulikofanyika unyama huu. Lakini nikaambiwa hawaoni juhudi za viongozi kumsaka mtuhumiwa.

“Nikatafuta namba katika simu yangu, nikakuta namba nimeandika kiongozi wala simjui nikampigia kumjulisha, akaniomba namba za viongozi wa kijiji, nikatafuta nikampa akaahidi kulifuatilia,” anasema.

Mtoto huyo alifanywa ukatili huo baada ya mtuhumiwa kwenda nyumbani kwao anakoishi na babu na bibi na kumlaghai ampeleke shambani aliko babu, ndipo akampeleka porini na kumfanyia hivyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live