Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sakata la watoto kuchinjwa Njombe ni mshikemshike

39303 Watotopic Sakata la watoto kuchinjwa Njombe ni mshikemshike

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Njombe. Wakati Umoja wa Mataifa (UN) ukitoa taarifa kulaani matukio ya mauaji ya watoto wilayani hapa, Serikali imeagiza kikosi kazi maalumu cha Jeshi la Polisi kufika Njombe ili kuongeza nguvu ya kuwasaka wanaojihusisha na ukatili huo.

Jana, naibu waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Hamad Masauni alikutana na waganga wa tiba asili na mbadala Mkoa wa Njombe kujadili mauaji hayo yanayohusishwa na imani za kishirikina huku watoto wapatao 10 wakiripotiwa kuchinjwa na kunyofolewa baadhi ya viungo.

Baada ya waziri huyo kusikiliza hoja za wataalamu hao wa tiba asili ambao waliilalamikia Serikali ya Mkoa wa Njombe kusambaratisha umaoja wao, walitaja vyanzo vingine vinavyoweza kuchangia mauaji hayo, mambo yaliyomfanya kuagiza kikosi hicho maalum cha jeshi.

Kikao cha waganga wa jadi

Akizungumza katika kikao hicho cha waziri, mlezi wa Chama cha Waganga wa Tiba Asili na Mbadala (CCWI) Mkoa wa Njombe, Antony Mwandulami alisema hapakuwa na matukio kama hayo kwani walijisimamia wenyewe kwa kushirikiana na Serikali.

Mlezi huyo ambaye ni mkazi wa Wangamba-Makambako, alisema umoja wao ulivurugwa na kiongozi mmoja wa Serikali mkoani hapa kwa kuruhusu kuingiza waganga kutoka nje ya mkoa na kuwapa leseni bila kuwashirikisha.

“Niseme hivi, mimi nina miaka 30 nipo kwenye shughuli hii ya uganga wa jadi ambao ni urithi kutoka kwa baba yangu. Hakuna mtu yeyote anayeweza kupata utajiri eti kwa kuua watu au kutumia viungo vya binadamu hilo halipo,” alisema Mwandulami.

Alisema licha ya uwezekano wa matukio hayo kufanywa na waganga feki, alidokeza kwamba matukio hayo wilayani Njombe yanaweza pia kuchangiwa na migogoro ya ardhi ndani ya familia, mirathi, ndoa na visasi, hivyo vyombo vya dola vinahitaji umakini zaidi katika kuyakomesha.

Alisema, “Kwa mfano, huyu mwenzetu aliyepoteza watoto watatu (Danford Nziku) wa Kijiji cha Ikando, wakati mmoja alikuwa na migogoro ya mashamba na ndugu yake ambaye amekamatwa. Yeye mwenyewe miaka michache iliyopita alinusurika kuuawa kwa kuchoma moto na ndugu yake huyohuyo na hadi leo hii tairi lililokuwa litumike kumchoma moto lipo kwangu pale.”

Chifu wa Kabila la Wabena, Elias Mkongwa alisema ni jambo la kusitikisha kuona viongozi wa Serikali wakivunja utaratibu wa usajili na uingizwaji wa waganga wa jadi tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambako machifu walishirikishwa.

“Nasikitika sana na matukio haya. Inauma sana, sisi Iringa na Njombe hatujawahi kuwa na matukio haya kutokana na uongozi imara uliokuwapo. Hivyo nashauri Serikali ikutane na sisi na kutushirikisha katika mambo haya ili kuwadhibiti waganga wanaotumia leseni halali wanazopewa na Serikali ili kuhalalisha uhalifu kama huu,” alisema Chifu Mkongwa.

Kikosi maalumu

Baada ya kuwasikiliza waganga hao, Masauni alitoa maagizo matatu huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano kufanikisha operesheni ya kutokomeza mauaji hayo.

Kwanza alimtaka Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kutuma kikosi kazi maalumu kwenda Njombe ili kuongeza nguvu ya kuchunguza matukio hayo na kuwahoji watu wote wanaoshikiliwa ili kuunasa mtandao mzima wa biashara hiyo.

Alisema Serikali itaongeza nguvu ya msako ndani na nje ya Njombe hususani katika maeneo ya misitu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwamo waganga wa jadi waliosajiliwa.

Pili, aliutaka uongozi wa Mkoa wa Njombe kufanya uhakiki upya wa leseni za waganga wote wa jadi.

Pia alisema jingine litakalofanyiwa kazi ni jinsi ya kushughulikia matukio yanayohusiana na mauaji akirejea tukio la juzi ambalo maofisa wa Jeshi la Polisi walitoa taarifa tofauti hadharani juu ya sababu za kutumika kwa mabomu ya machozi kutawanya wananchi.

Wakati kaimu kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Rashid Ngonyani akisema askari waliingilia kati kumuokoa mshukiwa wa wizi wa pikipiki aliyekuwa akifukuzwa na madereva wengine wa pikipiki, kaimu mkuu wa kituo cha Polisi Njombe, Kashoraeli Munuo alisema kuna mtu alikuwa anataka kumteka mtoto na wananchi wakawa wanamfukuza.

Taarifa ya UN

Juzi, Umoja wa Mataifa ulituma salamu za rambirambi kwa familia na ndugu waliopoteza watoto waliouawa huku ukisema mauaji hayo hayakubaliki kwani watoto wana haki ya msingi ya kulindwa dhidi ya vurugu ili waweze kufurahia na kupata mahitaji yao muhimu.

“Umoja wa mataifa unaungana na Serikali ya Tanzania kupinga vitendo hivyo vibaya. Kama UN tupo tayari kusaidiana na Serikali katika jitihada za kukabiliana na tatizo hilo,” anaeleza taarifa hiyo ikimnukuu mratibu mkazi wa UN Tanzania, Alvaro Rodriguez.

“Zaidi ya hayo tunatoa wito kwa wadau wote kuungana pamoja kuhakikisha kunakuwa na usalama wa watoto kuanzia katika makazi, shule na maeneo mengine.”

Mbali ya Rodriguez, taarifa hiyo pia imemkariri mwakilishi wa Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) nchini, Maniza Zaman akisema, “Watoto wanapitia katika aina nyingi za unyanyasaji katika maeneo mengi duniani. Hili linatakiwa likome.”

Kilio cha mzazi

Tangu taarifa za kushika kasi kwa matukio hayo zilipotangazwa, Serikali wilayani Njombe ilitoa amri kwa wazazi na walezi kuwapeleka na kuwafuata watoto wao shule.

Mmoja wa wazazi hao, Bahati Yovela wa Mji Mwema alisema licha ya vyombo vya dola kuendelea kuwahakikishia usalama na kukomesha matukio hayo, “Shughuli za uzalishaji zinakwama. Sasa ninalazimika kuchelewa kwenda kazini kwa ajili ya kumpeleka mwanangu na mchana ninawahi kurudi ili kwenda kumchukua.”

Watoto 10 wachinjwa Njombe

Wizara ya Afya yalaani mauaji ya watoto Njombe



Chanzo: mwananchi.co.tz