Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sakata la mwanakwaya kufia gesti, ndugu watumiwa meseji za vitisho

16256 Sakata+pic TanzaniaWeb

Sun, 9 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar. Mtu anayedaiwa kumuua Mariam Charles (22), mwanakwaya wa Kanisa la AICT, Chang’ombe ameendelea kuwatumia ndugu wa marehemu ujumbe mfupi.

Mwili wa Mariam ulikutwa kwenye nyumba ya wageni ya East London, Buza anakodaiwa alikuwa na mchumba wake usiku wa kuamkia Jumatano iliyopita.

Mariam na mchumba wake, wote walikuwa waimbaji wa kwaya ya vijana ya Kanisa la AICT Chang’ombe (CVC) inayotamba na albamu ya Pazia la Hekalu.

Mariam alikutwa amefariki dunia ikiwa ni siku chache kabla ya kutolewa mahari tukio ambalo lilipangwa kufanyika jana. Akizungumzia ujumbe huo, dada wa marehemu, Lucy Enock alisema baadhi ya wanafamilia wametumiwa meseji za vitisho kwa mtu anayedhaniwa kuwa ni muuaji anayetumia simu ya marehemu Mariam.

“Jana jioni nimetumiwa meseji na amekuwa akitutishia,” alisema ametumiwa ujumbe kwa namba ya Mariam unaosema: “Nimemuua Mariam kwa ajili ya uongo wake kwangu na alinitengenezea njama kwa mama (anamtaja jina) ili nikamatwe, nikamgundua baada ya mama huyo kumpigia akiwa anaoga...” Lucy alisema kifo cha mdogo wake kimeacha simanzi kwani mbali na huduma yake ya uimbaji, alikuwa akiishi vizuri na jamii wakiwamo wazazi wake.

Ndugu mwingine wa marehemu, Paul Makelele alisema amepokea vitisho kutoka kwenye namba ya Mariam.

“Kuna meseji nimetumiwa, inasema; “Mtindo wangu wa kushindwa kutunza siri nina silaha au nikufuate? Ni meseji nyingi napokea,”alisema.

Meseji nyingine aliyotumiwa ilisema:

“Jamani kama kukimbia ningeweza, maana nilikuwa nimefika nje ya mji, saa hivi nimerudi naenda polisi mwenyewe, hata kujiua nashindwa hata nikijaribu kwa sababu sijaua kwa kukusudia.” Ujumbe huo mfupi uliendelea kusema: “Ni bora kuuliwa kuliko mateso ya nafsi ya Mariam ninayoyapata. Mariam ananitokea kila nikitaka kujiua...”

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema wanaendelea kufanya uchunguzi.

Mama mzazi wa marehemu, Ester Charles amesimulia namna alivyopata taarifa za binti yake kuuawa siku chache kabla ya kulipiwa mahari.

Akizungumza na waandishi wa Mwananchi waliofika msibani hapo, mama huyo alisema Septemba 4 mwanae alimuaga kuwa anaenda kanisani kwenye kwaya.

“Baadaye akaniambia ameitwa na mchumba wake hivyo anaenda kuonana naye. Sikuwa na wasiwasi kwa sababu ni mchumba wake na binti alikuwa akiaga popote anapoenda,” alisema. Alisema baadaye alishangaa kupata ujumbe kutoka kwa mchumba wa mtoto wake unaosema; “Tayari nimemuua mwanao... Nilishtuka na ikabidi tuanze kumtafuta Mariam. Tukaenda polisi. Kusema kweli tangu hapo hali yangu nikawa sielewi hadi tulipokuja kuona kweli amemuua,” alisema na kuongeza:

“Binti yangu alikuwa mpole, mnyenyekevu, hana ugomvi na mtu na aliniaga kila anakoenda.”

Chanzo: mwananchi.co.tz