Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sakata la bastola mbele ya RC, RPC

38334 Bastola+pic Sakata la bastola mbele ya RC, RPC

Fri, 25 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Polisi mkoani Kilimanjaro imedai kuendelea na uchunguzi wa tukio la kutolewa kwa bastola mbele ya wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja sasa.

Tukio hilo linadaiwa kutokea Desemba 26, 2018 katika klabu moja maarufu ya usiku, hatua chache kutoka alipokuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira na kamanda wa mkoa, Hamis Issah.

Mfanyabiashara wa magari jijini Dar es Salaam, Emmanuel Kisoka anadaiwa kumtolea bastola mfanyabiashara mwenzake wa Moshi, Baraka Olotu. Hata hivyo, Kisoka amekanusha madai hayo.

Tukio hilo limekuwa gumzo mjini Moshi na kuibua maswali ya kutaka uwapo wa udhibiti wa uingiaji na silaha katika kumbi za starehe.

Issah alipoulizwa jana kuhusu taarifa zilizozagaa kuwa katika ukaguzi polisi walikuta risasi moja ikiwa chemba, alisema ni uzushi na upelelezi unaendelea.

“Hizo taarifa ambazo mnanipa naweza kusema ni uzushi maana sisi hatukijui hicho mnachokisema ndiyo maana kuna uchunguzi tunaufanya kuhusiana na hilo tukio,” alisema.

Kamanda Issah alifafanua kuwa mtu yeyote anayemiliki bastola au bunduki anaweza kuweka risasi chemba kwa kujihadhari kutegemeana na utaalamu wake na umakini alionao.

Hata hivyo, Kisoka alikaririwa na gazeti hili wiki iliyopita akikiri kuwapo kwa purukushani ndani ya klabu hiyo lakini akakanusha kuchomoa bastola hiyo bali walinzi ndiyo waliohamaki baada ya kuiona.

“Hii issue (suala) ikitokea hata RPC alikuwapo. Nilikuwa naamua tu ugomvi kati ya Olutu na vijana fulani ndiyo wale ma bouncer (walinzi) wakaiona waka-panic (kuhamaki),” alisema

Kisoka alidai bastola hiyo anaimiliki kihalali kwa ulinzi binafsi, baada ya walinzi kuiona akiamua ugomvi waliwaita polisi waliokuwa nje.



Chanzo: mwananchi.co.tz