Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sabaya kizimbani tena kwa Uhujumu Uchumi, kesi kuendeshwa wiki nzima

SABAY ED (2).jpeg Lengai Ole Sabaya, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai

Mon, 18 Oct 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kesi ya uhujumu uchumi namba 27 inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita, itaendelea kuunguruma leo Oktoba 18,2021 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwa wiki nzima mfululizo.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni Silvester Nyengu (26), Enock Togolani (41), Watson Mwahomange (27), John Odemba, Jackson Macha (29) na Nathan Msuya (31) wanakabiliwa na mashtaka matano.

Hadi sasa mashahidi wa tatu wa Jamhuri katika shauri hilo, wameshapanda kizimbani kutoa ushahidi wao wa msingi mahakamani humo.

Shtaka la kwanza, kwenye kesi hiyo ni la kuongoza genge la uhalifu kinyume na Sheria ya Uhujumu Uchumi Kifungu cha 57 (1) na 60 (2) na linawakabili washtakiwa wote.

Shtaka la pili, ni la kujihusisha na vitendo vya rushwa na linamkabili mshtakiwa wa kwanza peke yake, na ni kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Kifungu cha 15 (1B,2) sura ya 329 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Shtaka la tatu, ni la kujihusisha na vitendo vya rushwa, linamkabili mshakiwa wa kwanza peke yake, kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kifungu cha 15 (1B,2) sura ya 329 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Shtaka la nne, ni la matumizi mabaya ya madaraka, linalomkabili Sabaya peke yake, kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Shtaka la tano, la utakatishaji wa fedha na linawakabili washtakiwa wote saba, ni kinyume na kifungu 12 (D),13 (1A), cha Sheria ya Utakatishaji Fedha sura ya 423 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live