Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sabaya anavyoruka viunzi Mahakamani!

Rufani Ya DPP Dhidi Ya Sabaya Kusikilizwa Leo Sabaya anavyoruka viunzi Mahakamani!

Sun, 19 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Arusha. Hatimaye aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili wameshinda rufaa ya pili ya kesi iliyokuwa imekatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Rufaa hiyo ya jinai namba 231/2022 ilikuwa inapinga uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, uliowaachia huru Sabaya na wenzake wawili ambao ni Sylvester Nyegu na Daniel Mbura.

Ushindi huo, unafuatia rufaa ya kwanza ya Mei 6, 2022, ambapo Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, mbele ya Jaji Sedekia Kisanya aliwafutia hatia Ole Sabaya na wenzake, baada ya kuhukumiwa kwenda jela miaka 30 kwa makosa ya unyang'anyi wa makundi.

Baada ya Sabaya na wenzake kupangua rufaa hizo mbili, sasa wamebakiwa na rufaa nyingine moja namba 155/2022 ya kesi ya uhujumu uchumi inayowahusisha pia Enock Mnkeni, Sylvester Nyegu, Joh Aweyo, Jackson Macha na Nathan Msuya, isipokuwa Watson Mwahomange.

Awali Oktoba 15, 2021 Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo, aliwahukumu Sabaya na wenzake kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya unyang'anyi wa makundi, kwani Jamhuri ilishindwa kuthibitisha makosa ya unyang'anyi wa kutumia silaha waliyokuwa wameshitakiwa nayo awali.

Kesi zilivyoanza

Sabaya alisimamishwa kazi ya ukuu wa Wilaya ya Hai na Rais Samia Suluhu Hassani Mei 13, 2021 kupisha uchunguzi kabla ya kukamatwa Mei 27 mwaka huo wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Juni 4, 2021 Sabaya na wenzake watano walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha na kusomewa mashitaka sita tofauti, kesi ambazo zilikuja kusikilizwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Mashitaka hayo yalikuwa manne ya uhujumu uchumi na mawili ya unyang’anyi wa kutumia silaha kwenye kesi mbili tofauti zilizosikilizwa na mahakimu tofauti.

Washitakiwa wengine ni pamoja na Nyegu, Mnkeni, Mwahomange, Aweyo na Mbura.

Kesi ya kwanza jinai namba 66/2021 ilikuwa ya unyang'anyi wa kutumia silaha, yeye na wenzake wawili Nyegu na Mbura, walikuwa wakikabiliwa na makosa mawili ya unyang'anyi wa kutumia silaha na ilisikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Salome Mshasha.

Julai 16, 2021 Hakimu aliyekuwa akisikiliza shauri hilo alibadilishwa, ambapo alianza kusikiliza Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo kutoka mkoani Geita.

Baada ya watuhumiwa hao kufutiwa kesi hiyo walisomewa mashitaka mapya katika kesi ya jinai namba 105/2021 na kusomewa mashitaka matatu ya unyang’anyi wa kutumia silaha, ambayo baadaye kwenye hukumu walikuja kutiwa hatiani kwa makosa ya unyang'anyi wa makundi.

Akiwasomea upya mashitaka hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdallah Chavula, alidai kosa la kwanza ni unyang’anyi wa kutumia silaha linalowakabili washitakiwa wote watatu ambapo wanadaiwa Februari 9, 2021 katika Mtaa wa Bondeni jijini Arusha, waliiba Sh2.76 milioni mali ya mfanyabiashara Mohamed Saad.

Alidai kuwa kabla na baada ya kufanya wizi, waliwashambulia Numan Jasini, Harijin Saad Harijin, Bakari Msangi, Salim Hassan na Ally Shaban kwa kuwapiga na walitumia silaha aina ya bunduki ili waweze kupata mali hiyo.

Chavula alitaja shitaka la pili kuwa ni wizi wa kutumia silaha ambapo Februari 9, 2021 katika Mtaa wa Bondeni wanadaiwa kuiba fedha Sh390,000 mali ya Bakari Msangi ambaye ni Diwani wa Kata ya Sombetini na kabla ya kufanya tukio hilo walimfunga pingu, kumpiga na kumshambulia huku wakimtishia kwa kutumiabunduki.

Shitaka la tatu linalowakabili washitakiwa wote pia ni wizi wa kutumia silaha ambapo wanadaiwa katika mtaa huo waliiba Sh35,000 na simu ya mkononi aina ya tecno mali ya Ramadhan Rashid na kuwa baada ya wizi huo walimfunga pingu, kumpiga na kumtisha kwa bastola.

Kesi ya pili

Kesi ya pili ilikuwa ni ya uhujumu uchumi namba 27/2021 iliyokuwa ikimkabili Sabaya na wenzake watano ambao ni Nyegu, Mnkeni, Mwahomange, Aweyo, Macha na Nathan Msuya.

Walikuwa wakikabiliwa na mashitaka matano, yakiwamo ya rushwa mawili, moja la matumizi mabaya ya madaraka, kuunda genge la uhalifu na utakatishaji fedha.

Katika shauri hilo Sabaya peke yake alikuwa akikabiliwa na mashitaka manne na wenzake mashitaka mawili.

Mashitaka yaliyokuwa yanawakabili yalikuwa ni kushiriki vitendo vya rushwa na kumshawishi mfanyabiashara Francis Mrosso kuwapa Sh90 milioni ili kuepuka vitendo vya jinai walivyodai vinamkabili.

Ilipofika Oktoba 15, 2021, Sabaya na wenzake wawili waliokuwa wanakabiliwa na kesi namba 105/2021 walitiwa hatiani baada ya mahakama kuona wamethibitika kufanya unyang'anyi wa makundi na kuhukumiwa jela miaka 30 kila mmoja.

Hata hivyo, walikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kuipinga hukumu hiyo.

Ashinda rufaa ya kwanza

Mei 6, 2022 Mahakama Kuu Kanda ya Arusha mbele ya Jaji Sedekia Kisanya, iliwafutia hatia na kuamuru waachiwe huru baada ya kushinda rufaa yao ambapo pia waliendelea kukaa ndani kutokana na kuwa na kesi nyingine.

Wapangua kesi mpya

Aidha, Mei 30, 2022 Sabaya alifunguliwa kesi nyingine ya uhujumu uchumi namba 2/2022 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Moshi ambapo alishitakiwa yeye na wenzake Nyegu, Aweyo, Msuya na Antoro Assey.

Walisomewa mashitaka saba ya rushwa, mawili ukiukwaji wa utumishi wa umma (Sabaya pekee), kuongoza genge la uhalifu na utakatishaji fedha (kwa wote), mashitaka mawili kumsaidia Sabaya kushawishi kujipatia manufaa asiyostahili ya Sh30 milioni (kwa wenzake).

Waachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi

Juni 10, 2022 Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha mbele ya Hakimu Mkazi, Patricia Kisinda, Sabaya na wenzake sita walipangua kesi ya pili baada ya mahakama hiyo kuona kuwa hawana hatia.

Mahakama ilisema kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka yoyote, ikieleza ushahidi wake uligubikwa na utata na kwamba hati ya mashtaka ilikuwa na upungufu wa kisheria.

Kama hiyo haitoshi, Aprili 6, 2023 Sabaya aliachiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, kwa masharti ya kutofanya kosa la jinai kwa kipindi cha mwaka mmoja na kulipa faini ya Sh5 milioni baada ya kukiri kosa la kula njama na kuzuia utekelezaji wa haki.

Rufaa ya pili

Katika uamuzi uliosomwa juzi Novemba 17, 2023 na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa nchini, Abeesiza Kalegeya aliwaachia Sabaya na wenzake Nyegu na Mbura.

Hukumu hiyo ilitolewa na majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa wakiongozwa na Jaji Jacobs Mwambegele, Ignas Kitusi na Leiya Mgonya, waliosikiliza rufaa hiyo kwenye kikao chao kilichofanyika Arusha.

Akisoma uamuzi huo, Naibu Msajili huyo, alisema kuwa uamuzi uliofanywa na Mahakama Kuu ya Arusha wa kuwaachia washtakiwa hao, pamoja na kwamba haikuwa sahihi, lakini pia makosa ya unyang'anyi wa kutumia silaha yaliyobadilishwa na kufanywa ya unyang'anyi wa kikundi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha pia hayakuthibitishwa.

Hata hivyo, Sylvester Nyegu na Daniel Mbura hawakuwepo mahakamani wakati rufaa hiyo ikiamuliwa.

Rufaa ya tatu iliyobaki

Baada ya Sabaya na wenzake kupangua kesi hizo, kwa sasa wamebakiwa na rufaa nyingine moja namba 155/2022 ambapo mbali na Sabaya, wajibu rufaa wengine ni Mnkeni, Nyegu, Aweyo, Macha na Msuya.

Rufaa hiyo iliyokuwa inasikilizwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, inapinga Sabaya na wenzake kuachiwa huru ambapo Februari 20,2023 mawakili wa wajibu rufaa waliwasilisha maombi ya kufanya mapitio ya mwenendo wa rufaa hiyo katika Mahakama ya Rufaa.

Mbele ya Jaji Salma Maghimbi wa Mahakama Kuu aliyekuwa akisikiliza rufaa hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Felix Kwetukia, alieleza mahakama kuwa walipokea 'notice of motion' (maombi ya kufanya mapitio), yaliyoomba mahakama hiyo ya juu ifanye mapitio ya mwenendo wa rufaa hiyo na uamuzi mdogo uliotolewa Desemba 14, 2022 hivyo kuomba rufaa hiyo isubiri kwanza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live