Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

"Sabaya alikuwa na nia ovu" - Mkuu wa Upelelezi

Ebc4a530b2918f52b874b9f53ac1b051 Sabaya

Wed, 4 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SHAHIDI wa saba katika kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha na uporaji inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili amedai kuwa operesheni iliyoongozwa na Sabaya ilikuwa na nia ovu.

Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arusha, Mrakibu wa Polisi {ASP} Gwakisa Venance Minga [45} alisema katika Mahakama ya Hakimu mkazi Mkoa wa Arusha kuwa, operesheni ya washitakiwa katika duka la Shahiid Store katika mtaa wa Bondeni jijini Arusha haikuzingatia taratibu za upekuzi na ukamataji.

Minga alisema hayo wakati akiongozwa na mwanasheria mwandamizi wa serikali ,Abdallah Chavula mbele ya Hakimu Mwandamizi,Odira Amworo.

Sabaya, Silvester Nyengu na Daniel Mbura walidaiwa kutumia silaha kutesa na kupora mali na shilingi 3,159,000 Februari 9 mwaka huu.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali,Abdallah Chavula na Shahidi OC CID Minga;

Chavula;- Unaitwa nani

Shahidi; Naitwa Mrakibu {ASP} Gwakisa Venance Minga Mkuu wa Upelelezi Wlaya ya Arusha

Chavula;-Umehudumu Polisi kwa muda wa miaka mingapi

Shahidi; Miaka ishirini na moja polisi na miaka kumi na nane idara ya upelelezi

Hebu ieleze mahakama siku ya tarehe 9/2/2021 ulikuwa wapi majira ya saa 4 usiku

Shahidi; Muda huo nilikuwa Kituo Kikuu Cha Polisi Arusha katika majukumu yangu ya kawaida ya kikazi

Chavula;- Wakati ukiwa kituo Kikuu Arusha ni jambo gani lilitokea

Shahidi;- Nilipokea simu kutoka kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha Kenani Kihongosi.

Chavula;- Alikupigia simu akikutaka nini.

Shahidi;- Mkuu wa Wilaya ya Arusha Kenani Kihongosi alisema Mkuu wa Wilaya ya Hai,Lengai Ole Sabaya amekamata watuhumiwa hivyo angalia kama wana kesi ya jinai au la na nimpe mrejesho.

Chavula;- DC wa Arusha alikuambia ni watuhumiwa gani na wana makosa gani.

Shahidi;- Hakuniambia.

Chavula;- Baada ya taarifa ya Dc wa Arusha nini kilifuata.

Shahidi;- Nilitoa taarifa kwa OCD Mchunguzi na RCO Mwafulambo lakini na wao hawakuwa na taarifa yoyote juu ya taarifa ya kukamatwa kwa watuhumiwa na DC wa Hai na wote waliniambia nimsubiri huyo Mkuu wa wilaya ya Hai ajue watuhumiwa hao na baadae nitoe mrejesho kwao

Chavula;- Baada ya kupata maelekezo hayo nini kilifuata

Shahidi;- Baada ya muda alikuja Dc wa Hai Sabaya akiwa na Msaidizi wake Silvester Nyengu na dereva ambaye hakumtambua jina wakiwa na watuhumiwa wawili vijana walionekana kuwa ni waarabu

Chavula;- Hao vijana wawili waliokuja na mshitakiwa wa kwanza na wa pili mara ya mwisho uliwaona wapi

Shahidi;- Sijawahi kuwaona kabisa ndio ilikuwa mara yangu ya kwanza

Chavula;- Sabaya uliwahi kumwona wapi

Shahidi;- Niliwahi kumwona katika shughuli za kiserikali hivyo namjua

Chavula Silvester Nyengu uliwahi kumwona wapi.

Shahidi;- Nilikuwa namwona akiwa na DC wa Hai Sabaya mra kwa mara.

Chavula;- Unasema utaratibu wa kukamata watuhumiwa umekiukwa kivipi.

Shahidi;- Moja Mamlaka yake ya kikazi ni Wilaya ya Hai,hivyo kuja Arusha kukamata watuhumiwa kwanza alipaswa kushirikisha polisi na vyombo vingine vya ulinzi vya usalama lakini hilo halikufanyika na kwa kuwa halikufanyika tataribu zilikiukwa Sabaya alikuwa na nia ovu.

Chavula;- Uliwaona watuhumiwa hao

Shahidi;- Niliwaona na niliwahoji na watuhumiwa wa Sabaya walikuwa wameiva usoni na walionekana kupigwa sana.

Chavula;- Kwa nini unasema taratibu hazikufuatwa.

Shahidi;-Kwa sababu ukamataji wa watuhumiwa ,kupekuliwa ,kuporwa mali na fedha zao na kama taratibu zingefuatwa yote hayo yasingekuwepo

Kesi hiyo haikuendelea jana kwa kuwa Sabaya hakufika mahakamani. Mkaguzi wa Magereza, Ramadhani Msanga aliieleza mahakama kuwa Sabaya anajisikia vibaya kiafya na alipewa mapumziko ya siku moja (jana).

Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali,Tumaini Kweka alisema kwa kuwa mshitakiwa wa kwanza ni mgonjwa na hakufika mahakamani kisheria chini ya kifungu 196 inayosimamia mwenendo wa mashauri ya jinai sura ya 20 kuwa usikilizwaji wa ushahidi inaeleza lazima mshitakiwa awe mahakamani.

Hakimu Amworo alihairisha kesi hiyo hadi kesho (5 Agosti, 2021).

Chanzo: www.habarileo.co.tz