Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sabaya akiri alikuwa Arusha siku ya tukio

D20f2001d3538fbed7fc599c9b5ac2ac Sabaya akiri alikuwa Arusha siku ya tukio

Thu, 19 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MSHITAKIWA wa kwanza katika kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha na uporaji wa mali na zaidi ya Sh 3,159,000, Lengai Ole Sabaya (34) amesema Februari 9, mwaka huu alikuwa jijini Arusha kwa kazi maalumu.

Wakati huo Sabaya alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.

Mshitakiwa huyo na wenzake wawili, Silvester Nyengu (26) na Daniel Mbura (38) wanakabiliwa na mashitaka ya kutumia silaha kupora katika duka la Shahiid Store linalomilikiwa na Mohamed Al Saad katika mtaa wa Bondeni, jijini Arusha.

Sabaya alisema jana mahakamani kuwa, Februari 9, mwaka huu alikuwa katika mtaa wa Soko Kuu jijini Arusha katika operesheni maalumu akiwa na watu wanne kutoka Dar es Salaam.

Alisema walikwenda huko kumkamata Mohamed Al Saad Hajirini kwa tuhuma ya kufanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni na kuuza bidhaa bila kutoa risiti.

Sabaya lisema hayo wakati akihojiwa na Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Baraka Mgaya mbele ya Hakimu Mwandamizi, Odira Amworo, ambapo alikana kulifahamu duka la Shahiid Store lililopo mtaa wa Bondeni, jijini Arusha.

Alidai katika operesheni hiyo aliwakamata vijana wawili na aliwapeleka katika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha.

Sabaya alidai Februali 9, mwaka huu saa 11:00 jioni hakuwa katika duka la Shahiid Store kama inavyodaiwa, bali alifika Arusha saa 12:00 jioni kwa kazi maalumu iliyoshirikisha watu wanne kutoka Dar es Salaam.

Alidai aliwapokea watu hao katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Alipotakiwa kutaja eneo walipokwenda katika mtaa wa Soko Kuu Arusha, Sabaya alidai hawezi kulisema kwa kuwa ilikuwa kazi maalumu.

Mgaya alimuhoji Sabaya kwa nini mawakili wake, Dancan Oolla na Mosses Mahuna hawakumuuliza shahidi namba sita katika kesi hiyo, Bakari Msangi (38) kuhusu hila za kisiasa kwa yeye kufunguliwa kesi, alidai hakuona sababu za kuuliza swali hilo.

Sabaya alikiri kumfahamu mshitakiwa wa pili, Nyengu kwa sababu alipangiwa kazi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, ila hafahamu ni katika idara ipi.

Aliwakana mashahidi namba 2,4, 6 waliodai kuwa siku ya tukio alikuwepo katika duka ulipofanyika uporaji.

Chanzo: www.habarileo.co.tz