Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sabaya aibuka na hoja 14 kupinga kifungo cha miaka 30

83712cf8d7abf2622cfee9386a6c6049.jpeg Lengai Ole Sabaya, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai

Mon, 13 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mawakili wa utetezi katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya (34) na wenzake wawili wamewasilisha hoja 14 katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kupinga hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela dhidi ya wateja wao.

Sabaya na Silvester Nyegu (26) na Daniel Mbura (38), Oktoba 15, mwaka huu walihukumiwa kifungo cha miaka 30 na Hakimu Mfawidhi Mwandamizi wa Mkoa wa Geita, Odira Amworo baada ya kukutwa na hatia ya makosa matatu ya kupora, kuiba na kutishia kwa silaha katika tukio lililotokea Februali 9, mwaka huu katika duka la Shahiid Store mkoani Arusha.

Mawakili wa utetezi wakiongozwa na Mosses Mahuna wametoa sababu 14 kupinga hukumu hiyo, wakidai Hakimu alipotoka katika kutoa uamuzi huo. Rufaa ya Sabaya namba 129 ya mwaka huu dhidi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) ilipokelewa Novemba 4, mwaka huu na Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha na leo inatarajiwa kutajwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

Sabaya, Nyegu na Mbura walikuwa wakikabiliwa na mashitaka matatu, la kwanza kuwa Februali 9, mwaka huu mtaa wa Bondeni jijini Arusha katika duka la Sahiid Store wakiwa na silaha walimpora Bakari Msangi Sh 390,000 na simu mbili na kabla ya uporaji walimshambulia kwa kumpiga ngumu, mateke, kofi, kichwa na kumtishia kwa silaha.

Shitaka la pili, Februali 9, mwaka huu Sabaya na wenzake walipora kaunta la duka hilo la Mohamed Al Saad kiasi cha fedha Sh milioni 2,769,000 na kabla ya uporaji walimpiga Jasin ngumi, mateke, kofi, kichwa na kumtisha kwa silaha na kiasi hicho cha fedha kutokomea nacho kusikojulikana. Shitaka la tatu la unyang’anyi wa kutumia silaha, Februali 9, mwaka huu mtaa wa Bondeni jijini Arusha wakiwa na silaha walimpora simu moja ya mkononi aina ya Tecno na Sh 35,000 Ramadhani Rashid na kabla ya kufanya hivyo, waliwalaza chini watu wote waliokuwa katika duka hilo na kuwapiga.

Katika hukumu iliyosomwa kwa saa 4.45 Oktoba 15, mwaka huu na Hakimu Amworo aliyetumia siku 37 kusikiliza kesi hiyo, alisema Mahakama imewakuta na hatia washitakiwa wote watatu baada ya kuridhishwa na ushahidi wa mashahidi wanne katika kesi hiyo. Alisema kwa mujibu wa sheria ya adhabu ya unyang’anyi wa kutumia silaha kifungu 287 (c), kila kosa adhabu yake ni miaka 30 jela na viboko 12 kila mmoja.

Alisema Sabaya na wenzake walikutwa na makosa katika kila shitaka ila mahakama imewaonea huruma na kuwafunga wote watatu miaka 30 jela.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live