Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu wadhamini kutaka Lissu akamatwe

96664 Lissu+pic Sababu wadhamini kutaka Lissu akamatwe

Mon, 24 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wadhamini wa makamu mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, katika kesi ya uchochezi inayomkabili wamebainisha sababu ya kutaka mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki akamatwe.

Wametaja sababu hiyo kuwa ni usumbufu wanaoupata kumpata mshtakiwa huyo aliyeko nchini Ubelgiji alikokwenda kutibiwa baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 akiwa kwenye makazi yake Area D jijini Dodoma.

Lissu pamoja na wenzake watatu, wanakabiliwa na kesi ya uchochezi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Taarifa zinasema mwanasheria huyo ameshamaliza matibabu lakini hajarudi nchini kwa madai ya kuhofia usalama wake.

Hali hiyo imesababisha kesi inayomkabili kushindwa kuendelea kutokana na kutokufika kwake, huku mahakama ikiwapa wadhamini wake jukumu la kumpeleka fkwa mujibu wa masharti ya dhamana aliyopewa.

Baada ya juhudi za wadhani hao, Robert Katula na Ibrahimu Kipepe kumpata kushindwa, jana waliwasilisha maombi ya kutaka mahakama itoe amri ya kumkamata Lissu popote alipo ili afikishwe mahakamani kuendelea na kesi.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Kwa mujibu wa hati ya kiapo cha maombi hayo, Katula anasema kwa jinsi mazingira ya kesi yalivyo, mahakama inahitajika kutumia mamlaka yake kuwezesha Lissu kuhudhuria kesi yake.

Katula anadai ikiwa amri ya kumkamata Lissu na kumfikisha mahakamani hapo haitatolewa, wataathirika kwa haki itakuwa haitendeki dhidi yao.

Katula anadai kuwa baada ya Lissu kushambuliwa alisafirishwa kwenda nje ya nchi kwa siri bila yeye (mdhamini) wake kujulishwa.

Anasema alifahamu uamuzi huo kupitia vyombo vya habari hasa magazeti, taarifa ambazo baadaye zilithibitishwa na Spika wa Bunge kupitia Shirika la Utangazaji nchini (TBC).

Hakimu Thomas Simba alipanga kusikiliza maombi hayo leo baada ya kupitia sheria zinazohusua suala hilo, huku akisisitiza kuwa maombi hayo na kesi ni vitu viwili tofauti.

Alisema amri alizokwishato kwa wadhamini hao kuhakikisha mshtakiwa anafika mahakamani zinabaki kuwa na nguvu ileile.

Amri ya mahakama

Desemba 19,2019 mahakama hiyo ilitoa amri kwa wadhamini hao kuhakikisha Lissu anafika mahakamani.

Katika utetezi wake, Katula alisema “tumefanya juhudi ya kuwasiliana na mshtakiwa, akasema anawasiliana na wakili wa chama baada ya hapo akawa kimya. Tukalazimika kumwandikia barua (Freeman) Mbowe, mwenyekiti wa Chadema kwa kuwa ndiye aliyemtoa nje ya nchi,” alidai Katula.

Alidai kuwa wakati anamdhamini mtuhumiwa hakujua kama mshtakiwa huyo angepigwa risasi na juhudi walizofanya ni pamoja na kuwasiliana na mwenyekiti wake wa chama wakitaraji zinaweza kuzaa matunda lakini haikuwezekana.

Wadhamini hao waliwasilisha nakala ya barua waliyomwandikia Mbowe kumuomba awasaidie kumrejesha Lissu nchini na kudai kuwa endapo atawasili wanaweza kumpeleka mahakamani.

Wakili wa Serikali Silvia Mitanto alisema jukumu la kuhakikisha mshtakiwa anafika mahakamani ni la mdhamini mwenyewe.

“Wadhamini hawa walikubali kumwekea dhamana na wakaridhia, kama ni kujitoa wangejitoa kabla mshtakiwa hajaenda nje ya nchi,” alisema Mitanto.

Hakimu Simba aliwataka wadhamini hao kuhakikisha mshtakiwa anapelekwa mahakamani kabla mahakama hiyo haijatoa amri nyingine.

“Usifikiri tutakusamehe jukumu lako ndiyo hilohilo, mtuletee mshtakiwa kwa kuwa jalada hili halijui hofu, huo ndio mkataba wako,” alisema Hakimu Simba na kisha akaahirisha kesi hiyo hadi jana, Februari 20.

Novemba 29, 2019 wakati Lissu akihojiwa na kituo cha televisheni cha KTN cha Kenya, alisema angerenjea Tanzania baada ya marafiki zake kumhakikishia usalama wake.

“Hali ya usalama wangu bado si nzuri, nafikiri hakuna mtu anayetaka kuona narudi nyumbani kesho na keshokutwa nikapigwa risasi tena,” alisema Lissu.

“Bado kuna vitisho vya aina hii, watu wenye busara lazima wakae na kuangalia namna nzuri ya kufanya ili niweze kurudi nyumbani kuendelea na shughuli zangu lakini nikiwa salama.”

Lissu na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya 1976.

Mbali na Lisu, washtakiwa wengine ni Mhariri wa Gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.

Kwa pamoja washtakiwa hao, wanakabiliwa pia mashtaka ya kuandika habari za uchochezi na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’

Chanzo: mwananchi.co.tz