Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu mgambo wa Makonda kunyimwa dhamana

16325 Mgambo+pic TanzaniaWeb

Sun, 9 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imezuia dhamana dhidi ya washtakiwa watatu wanaokabiliwa na shtaka la kujeruhi, wakiwamo mgambo wawili wa Jiji la Dar es Salaam.

Washtakiwa waliozuiliwa dhamana katika kesi hiyo ya jinai namba 277/2018 ni mtendaji wa kata ya Bunju, Ibrahim Mabewa (39) mkazi wa Madale.

Wengine ni Kelvin Sawala (25) mkazi wa Wazo na Gudluck Tarimo (30) mkazi wa Kimara, ambao ni mgambo wanaosimamia operesheni usafi katika Jiji la Dar es Salaam.

Hatua hiyo ilitokana na upande wa mashtaka kuiomba mahakama hiyo kuzuia dhamana kwa sababu za usalama dhidi ya washtakiwa hao na muathirika wa tukio hilo, hali yake si nzuri.

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa shtaka linalowakabili.

Wakili wa Serikali mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi akisaidiwa na Nasoro Katuga na Mwanaamina Kombakona, alidai washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka la kujeruhi.

Kombakona alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mahira Kasonde, kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo Agosti 30 eneo la Bunju wilayani Kinondoni.

Aliendelea kudai kuwa siku ya tukio, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kumpiga, Robison Oloth kwa kutumia rungu sehemu mbalimbali za mwili wake hivyo kumsababishia majeraha mbalimbali.

Washtakiwa walikana shtaka na kuiomba Mahakama iwapatie dhamana kwa sababu shtaka linalowakabili linadhaminika.

Hata hivyo, Katuga alidai kuwa upelelezi haujakamilika na hawajapata ripoti rasmi ya kitaalamu inayoonyesha namna Oloth alivyojeruhiwa.

Katuga alidai upande wa mashtaka wamewasilisha mahakamani hapo maombi ya kuzuia dhamana dhidi ya washtakiwa kwa sababu mbili; tukio lipo katika mitandao ya kijamii hivyo ni hatari kwa washtakiwa.

Aliendelea kuwa upande wa mashtaka wanaona siyo salama kwa washtakiwa kuwa nje kwa dhamana wakati jamii, ndugu wa mlalamikaji wakiwa na hasira dhidi yao.

“Ni busara kwa Mahakama kupitia kifungu cha sheria namba 148 (5) (d) cha Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA) ambacho kinazuia dhamana ya washtakiwa hadi hali ya usalama dhidi ya washtakiwa itakapoimarika,” alieleza.

Baada ya kusikiliza maombi ya pande zote, Hakimu Kasonde alisema Mahakama imezuia dhamana kwa washtakiwa hao kwa kuwa muathirika bado ni mgonjwa na yupo chini ya uangalizi wa madaktari Hospitali ya Sinza. “Kwa misingi hiyo, dhamana imezuiliwa mpaka pale mahakama itakapojiridhisha,” alisema.

Aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 20 itakapotajwa na washtakiwa walirudishwa rumande.

Mgambo wa Makonda kizimbani, wakosa dhamana

Chanzo: mwananchi.co.tz