Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na wenzake watatu leo Alhamisi Januari 20, 2021 imeahirishwa baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuleta shahidi wa 11 kama mahakama ilivyoamuru jana.
Jaji Joachim Tiganga alielekeza upande wa mashitaka kuandaa shahidi huyo kutokana na shahidi wa kumi Inspekta Inocent Ndowo kumaliza ushahidi wake mapema.
Baada ya upande wa Jamhuri kumaliza kumuhoji shahidi huyo kutokana na hoja zilizoibuka wakati upande wa utetezi wakimuhoji Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando alidai hawana shahidi mwingine kwa sababu shahidi waliyemtegemea jana hakuweza kupatikana na shahidi mwingine leo ndio anasafiri kuja Dar es Salaam.
Wakili Kidando: Mheshimiwa Jaji shauri linakuja kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa na tulikuwa tunaendelea na re- examination na tuko tayari kuendelea
Jaji: Utetezi?
Kibatala: Na siye Mheshimiwa Jaji tuko tayari kuendelea
Jaji: Shahidi nakumbusha uko chini ya kiapo na bado utaendelea kutoa ushahidi chini ya kiapo
Sasa Wakili wa Serikali Mwandamizi Kidando: Shahidi jana uliulizwa na wakili Nashoni Nkungu kama ni haki kudukua mawasiliano ya mtu ukasema ndio au hapana, ieleze Mahakama ulikuwa unamaanisha Nini?
Shahidi: Mheshimiwa nilikuwa namaanisha kuwa inategemeana na kile anachokifanya mtu, kama anafanya kwa nia ovu jibu ni hapana
Wakili: Uliulizwa pia uchunguzi ulioufanya Kama uliweza kubaini kuwa wanahusika na ugaidi ukasema mpelelezi ndio anaweza kujua hebu ieleze mahakama ulikuwa unamaanisha nini?
Shahidi: Mheshimiwa role yangu Kama mchunguzi ni kumpa mpelelezi kile alichoniomba yeye ndo anaweza kujua kinamsaidiaje, kwa hiyo kwa nafasi yangu siwezi Ila mpelelezi
Wakili: Uliulizwa pia Kama katika uchunguzi wako uliweza kubaini sauti za mawasiliano lakini ukasema kuwa wewe huwezi, hebu ieleze Mahakama
Shahidi: Kuna mtu wa tatu anayewaunganisha ambaye ni mtoa huduma. Kwa hiyo mto huduma ndiye anaweza kuwa na sauti, mimi ninachoweza kupata ni call log tu.
Shahidi: Mheshimiwa Jaji sisi tunachunguza vifaa vilivyoletwa kwa ajili ya uchunguzi na mwisho tunatoa taarifa kama walivyoomba.
Wakili Kidando: Shahidi uliulizwa maswali kuhusu kielelezo P6 barua uliyoiandika kwenda Tigo kuwa haina saini yako nawe ukasema kweli hukusaini, hebu ieleze Mahakama ni kwa nini hukusaini?
Shahidi: Kwa taratibu za kiofisi kwa cheo changu siwezi kusaini barua inayotoka nje ya Jeshi.
Wakili Kidando: Mheshimiwa Jaji baada ya shahidi huyu kwa leo hatuna shahidi mwingine, hivyo tunaomba ahirisho mpaka kwsho tarehe 21/2022.
Wakili Kidando: Kwa leo hatuna shahidi mwingine kwa sababu shahidi tuliyemtegemea jana hakuweza kupatikana na shahidi mwingine leo ndio anasafiri kuja Dar es Salaam. Shahidi tuliyemtegemea jana si mkazi wa Dar es Salaam na shahidi tunayemtegemea leo pia si mkazi wa Dar es Salaam.
Jaji: Upande wa mashtaka?
Wakili Kibatala: Mheshimiwa Jaji kama ambavyo amri yako ilielekeza Jana na mara kwa mara ni kuandaa mashahidi ili tuweze kuendelea maana sisi tupo, lakini kumekuwa na ucheleweshaji. Kwa hiyo sisi tunaiachia mahakama yako
Jaji: Naomba nitoe amri ya Mahakama hii Juzi na Jana. Labda kwa Jana ilikuwa ngumu kwamba shahidi huyu sehemu kubwa ya ushahidi mwingi alikuwa hajautoa, lakini kwa leo ilitegemewa kuwa shahidi leo angemaliza mapema lakini upande wa mashtaka umesema shahidi waliyemtegemea jana hakuweza kufika na wakamtafuta shahidi mwingine ambaye naye hakuweza kufika kwa kuwa mashahidi wote wanatoka nje ya Dar es Salaam.
Jaji: Lakini pia mahakama hii imesikiliza concern ya Upande wa utetezi. Mahakama hii imekuwa ikiendesha kwa spirit ya kumaliza kesi hii mapema.
Jaji: Kwa hiyo bila kusema mengi, mahakama hii inatoa amri kuwa upande wa mashtaka kesho uje na shahidi ili kesi iweze kuendelea. Lakini pia inaamuru Upande wa mashtaka pale ambapo Kuna dharura shahidi mmoja hawezi kufika itoa taarifa mapema na iandae shahidi mwingine wa kuchukua nafasi ili kuendelea na kesi.
Kwa hiyo ninaahirisha kesi hii mpaka kesho, tarehe 21/1/2022. Washtakiwa mtaendelea kuwa chini ya uangalizi wa Magereza.