Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Saa 51 za mtoto aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha

20018 Pic+mtoto TanzaniaWeb

Mon, 1 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Siku moja baada ya mtoto Thomas Rwehumbiza (9) aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha kupatikana akiwa amejificha katika moja ya nyumba eneo la Kilungule jijini hapa, mapya yameibuka kuhusu maisha yake.

Thomas alipatikana juzi saa moja usiku akiwa katika nyumba hiyo ambayo haijamalizika kujengwa mali ya Kanisa Katoliki Kigango cha Mtakatifu Salome Parokia ya Mtakatifu Monica Kilungule, alikolala kwa saa 51 akihofia kurejea nyumbani kwao.

Mtoto huyo anayesoma darasa la pili katika Shule ya Msingi Kilungule, alipotea Jumatano iliyopita eneo la Kimara Bonyokwa, taarifa za walimu na baba yake mzazi Renatus Rwehumbiza, zikieleza kuwa hakurejea nyumbani baada ya kutoka shule.

Mwananchi lilipofuatilia taarifa za kupotea kwake shuleni, lilielezwa kuwa alimkamatwa na mwenzake wakiwa na CD zenye picha zisizofaa kutazamwa na watoto na walihojiwa maswali kadhaa na walimu kisha kutakiwa kufika shuleni hapo Alhamisi asubuhi wakiwa wameongozana na wazazi wao.

Akizungumza na Mwananchi jana, Thomas alisema rafiki yake aliyemtaja kwa jina moja la Joshua, ndiye aliyempeleka katika nyumba hiyo Jumatano jioni baada ya kuhofia kurudi nyumbani, akiamini angechapwa.

“Tulikamatwa na CD shuleni lakini hazikuwa zangu zilikuwa za Joshua, mwalimu alisema twende na wazazi na siku ya Alhamisi na mimi niliogopa kurudi nyumbani kwani nimekuwa nikipigwa,” alisema.

Thomas alisema baada ya kupelekwa katika nyumba hiyo, Joshua alimuahidi kuwa atakuwa akimpeleka chakula.

“Usiku ulipoingia alikuja Noeli rafiki yake Joshua akaniletea ugali uliokuwa kwenye mfuko wa Rambo,” alisema Thomas.

Noeli (11) alisema amemfahamu Thomas kupitia Joshua.

“Ninamfahamu Joshua na ndiye aliyeniambia kuna rafiki yake anateswa na mama wa kambo anahitaji msaada nimpelekee chakula. Niliiba ugali na mboga nyumbani nikapeleka, kufika nilimkuta anasikia baridi, nilirudi nyumbani nikamchukulia nguo zangu na nikaiba shuka la kaka nikampelekea ajifunike,” alisema Noeli.

Thomas alisema Alhamisi asubuhi alitoka nje ya nyumba hiyo kutafuta maji ya kunywa kwa kuwa muda huo Joshua alikuwa amekwenda shule.

Baada ya kutoka, mlinzi wa kanisa hilo Ansela Njovu alimuona na alimfukuza eneo hilo akimtaka aende shule kwa kuwa alikuwa na sare. Mlinzi huyo alisema mchana alimuona tena.

“Nilikuwa nasubiri mpaka jioni Joshua atoke shule ndio aniletee chakula, wakati mwingine aliniletea ugali na maharagwe na ubwabwa,” alisema Thomas.

Mlinzi huyo alisema juzi asubuhi alimuona tena lakini akiwa amebadili nguo na alipotaka kumkamata alikimbia.

Alivyopatikana

“Mchana nilifanikiwa kumkamata na baada ya kumhoji alisema hana baba na mama anayeishi naye ni wa kambo na hamtaki,” alisema Njovu.

“Baada ya kuhojiwa alitueleza kuwa kuwa anaishi Mabibo (anapoishi mama yake mzazi). Baadaye sana akasema anaishi maeneo haya (Bonyokwa) na hapo akamtaja Joshua. Kwa kuwa Mama wa Joshua tunamjua ndipo tukafanikiwa kumkutanisha na mzazi wake.”

Baba wa Thomas alipoulizwa kuhusu kunyanyaswa kwa mtoto huyo alikana akisema, “Hanyanyaswi isipokuwa nimekuwa nikimpiga ikiwa atachelewa kurudi nyumbani. Huyu mtoto ni mtukutu namwadhibu mara nyingi tu hata walimu wake shuleni wanafahamu kuhusu matatizo yake.”

Mama anayeishi na mtoto huyo Anna-Mery Rwehumbiza alipoulizwa kuhusu madai ya Thomas alisema, “Huyu mtoto hanyanyaswi hapa nyumbani, anapewa malezi kama watoto wengine na si mara ya kwanza kupotea. Agosti 29 alipotea na tulimtafuta, alirudi hapa nyumbani saa sita usiku kwa kuletwa na mtu alipoulizwa hakuwa na majibu ya uhakika.”

Awali, Joshua alieleza kuwa, “Thomas amekuwa akilalamika kuwa ananyanyaswa na mama yake wa kambo, niliona nimsaidie. Zile CD niliziokota na ilikuwa tukaangalie jioni.”

Kilio cha mama mzazi

Licha ya matukio hayo, Lucy Dembe ambaye ni mama mzazi wa Thomas alisema hajaonana na mwanaye kwa miaka mitatu.

Huku akilia machozi karibu muda wote wa mahojiano, mama huyo alisema, “Awali walikuwa wakiishi Mabibo (baba watoto wake), lakini walihama kwa kunikimbia nisimuone mwanangu. Ninaumia kwa sababu hata matukio ya mtoto siyajui nafanya kusikia hapa wanaponieleza. Mtoto alipotea Jumatano taarifa nimepewa Ijumaa sitendewi haki.” alisema Lucy.

Afya ya mama wa mtoto

aliyetekwa kimafia asema

Licha ya wazazi wa Idrissa Ally (13), mtoto aliyepotea Jumatano iliyopita baada ya kuchukuliwa na mtu asiyejulikana akiwa anacheza na wenzake kuwa na imani kwamba watampata akiwa hai, afya ya mama yake mzazi imedhoofika kutokana na tukio hilo.

Mama huyo, Leila Kombe alisema jana kuwa kadri siku zinavyozidi kwenda, hali yake kiafya inazidi kuwa mbaya na kuomba kwa yoyote atakayemuona mwanaye atoe taarifa.

Mbali ya ombi hilo, alimuomba Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola kuingilia kati suala hilo ili mtoto wake huyo apatikane.

Idrissa, mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Princes Gate alichukuliwa Jumatano iliyopita saa 11 jioni eneo la Tegeta Masaiti jijini hapa.

Mtoto huyo alichukuliwa na dereva mwanamume aliyekuwa katika gari aina ya Toyota IST, ambaye baada ya kuwafukuza marafiki waliokuwa wakicheza naye, alitoa kichupa kidogo kinachodhaniwa ni ‘spray’ na kumpulizia mtoto huyo na hatimaye kumuingiza katika mlango wa nyuma wa gari lake na kutokomea naye kusikojulikana.

“Sasa hivi miguu yangu yote imeishiwa nguvu, sina raha kabisa leo (jana) siku ya tatu mwanangu sijui alipo. Sijui anakula nini huko, nazidi kumuomba Mungu,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz