Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rushwa yampeleka raia wa Pakistan kortini

37164 Rushwapic Rushwa yampeleka raia wa Pakistan kortini

Fri, 18 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Raia wa Pakistani, Muhammad Hasnain Hyderi leo Alhamisi Januari 17, 2019 amefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la kutoa rushwa ya Sh2 milioni kwa ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Talib Kombo.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi, Wanjah Hamza, wakili wa Takukuru, Leonard Swai amedai kuwa mshtakiwa alitoa rushwa hiyo ili asaidiwe asitoe kodi kubwa.

Wakili Swai amedai Januari 15, 2019 maeneo ya mgahawa wa Best Bite mshtakiwa alitoa rushwa ya Sh2 milioni kwa Kombo ili amsaidie asitoe kodi kubwa huku akijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Baada ya kusomewa shtaka la kutoa rushwa katika kesi hiyo namba 18/2019, mshtakiwa alikana na upande wa mashtaka kudai kuwa upelelezi umekamilika na kuiomba  mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea hoja za awali.

Hakimu Hamza amesema dhamana ipo wazi kwa mshtakiwa na wadhamini wanapaswa kuwa wawili watakaosaini bondi ya Sh5 milioni.

Hata hivyo, mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kurejeshwa mahabusu.

Hakimu Hamza ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 31, 2019 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa tena.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz