Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rushwa ya ngono vyuoni haikubaliki

C34a6d53a545ec20502561c08300cce5 Rushwa ya ngono vyuoni haikubaliki

Thu, 1 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mapema mwaka huu ilifanya utafi ti kuhusu suala la rushwa ya ngono katika vyuo vikuu nchini na ikaendesha utafi ti huo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo, umebaini kwamba tatizo la rushwa ya ngono kwenye vyuo vikuu vilivyoshiriki lipo, na tatizo hilo ni kubwa na si la kupuuzwa.

Kwa mujibu wa utafiti huo, baadhi ya wahadhiri huomba rushwa ya ngono ili kuwasaidia wanafunzi wafaulu, kupatiwa hosteli, kupatiwa ufadhili wa ndani na nje ya nchi na kupatiwa ajira, lakini pia wanafunzi huomba rushwa ya ngono ili wasaidiwe ufaulu.

Matokeo ya utafiti huo yalionesha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya wahojiwa (wenye uelewa), walieleza uwepo wa rushwa ya ngono katika vyuo vikuu vilivyofanyiwa utafiti, hivyo kuthibitisha rushwa ya ngono ni tatizo katika vyuo vikuu.

Utafiti huo ulipendekeza serikali iwajibishe uongozi wa vyuo vikuu, kwenye kujenga mazingira wezeshi na salama kwa wanafunzi na wafanyakazi katika ngazi zote ili kuwezesha wanafunzi wa jinsi zote kupata na kufaidi haki ya elimu.

Aidha, utafiti huo, kwa uongozi wa vyuo ilipendekeza uboreshe mifumo ya udhibiti na uwajibikaji kwenye kuimarisha mifumo ya kusimamia maadili, mifumo ya utahini, mifumo ya kutoa taarifa na kulinda watoa taarifa pamoja na kuwajibisha watuhumiwa wa vitendo hivyo.

Tunaipongeza Takukuru kwa kuja na utafiti huo kutokana na ukweli kuwa katika siku za karibuni, tatizo la rushwa ya ngono limeanza kushika kasi nchini, hasa katika taasisi za elimu kuanzia shule za msingi na hadi vyuo vikuu.

Hili ni tatizo ambalo jamii kwa ujumla kuanzia ngazi ya familia, haina budi kukabiliana nalo na kuchukua hatua za kulikomesha, kwani ni tatizo ambalo siyo tu lina athari kwa utu, lakini pia katika mfumo mzima wa elimu na wa baadaye nchini kwa sababu vyuo vitazalisha wanafunzi wasio na uwezo kwa kupendelewa katika ufaulu.

Taifa kwa ujumla linapaswa kutambua kuwa rushwa ya ngono haikubaliki, hivyo wanafunzi hasa wa kike waelezwe umuhimu wa kusimama kidete kukataa aina hii ya udhalilishaji, kwa kujituma katika masomo yao na kukataa kujiona wanyonge kimasomo, lakini kwa wahadhiri, kujiepusha na vitendo hii vinavyowavunjia heshima wao wenyewe, vyuo vyao na taifa kwa ujumla kwa kuzalisha wahitimu wasio na uwezo kimasomo.

Tunaamini mapendekezo yaliyotolewa katika utafiti huu, yatafanyiwa kazi na mamlaka husika kwa nia ya kuhakikisha tatizo hili linapatiwa ufumbuzi wa haraka ili lisiendelee kuharibu mfumo wa elimu nchini, lakini pia kuathiri vijana ambako masomoni kwa sababu kujitumbukiza katika vitendo hivi viovu.

Chanzo: habarileo.co.tz