Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rushwa ya ngono imekithiri kwenye vyama vya siasa

86242 NGONO+PIC Rushwa ya ngono imekithiri kwenye vyama vya siasa

Fri, 29 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia  na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nchini Tanzania imetakiwa kuvimulika vyama vya siasa kwa madai rushwa ya ngono imekithiri kwenye kada hiyo.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Novemba 27, 2019 na mwanaharakati  Eva Kihwele katika mjadala uliowakutanisha wadau wa masuala ya jinsia kulekea siku 16 kupinga ukatili wa kijinsia uliobebwa na kauli mbiu ‘Kataa rushwa ya ngono, jenga kizazi chenye usalama’ uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Mjadala huo ulioandaliwa na Mfuko wa wanawake Tanzania (TWF) kwa kushirikiana na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) umelenga kuhamasisha mapambano ya vita dhidi ya rushwa ya ngono.

"Takukuru angazeni vyama vyote vya siasa, wanawake wenzetu wanadhalilika, wanavulia nguo mpaka wakitembea barabarani wanaonekana kama wapo uchi."

"Anagombea ili jina lipite anatakiwa kuvuliwa nguo, Takukuru tusaidieni huko," amesema Kihwele

Mkurugenzi wa Intelijensia kutoka Takukuru, Emmanuel Kiyabo amesema rushwa ya ngono ni kubwa kuliko rushwa ya pesa na asilimia 28 ya wanawake wanaofanya biashara ndogondogo na wanafunzi wa vyuo wanatumikishwa rushwa ya ngono.

Anasema wanawake wengi hawatoi taarifa kwa kuogopa kudhalilika na kuitaka jamii kupaza sauti kwani rushwa ya ngono inaua, unapoteza utu na inaleta msongo wa mawazo na kuhujumu uchumi.

Naye  Mkurugenzi wa Tamwa Rose Rueben amesema ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto nchini ni janga hasa kwa nchi za Afrika, hivyo inatakiwa mikakati madhubuti na ya ubunifu.

Maadhimisho ya siku 16 ya kupinga ukatili wa kijinsia yanalenga kutoa  fursa ya kutafakari na kujadili na kushirikishana mafanikio kupambana na ukatili wa kijinsia pamoja na kujenga mikakati na sauti ya pamoja.

Chanzo: mwananchi.co.tz