Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rugemalira agonga mwamba

4312 RugemalirAA Rugemalira agonga mwamba

Fri, 8 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imetupilia mbali hoja za washtakiwa mfanyabiashara James Rugemalira na wenzake za kutaka kuondolewa mashtaka kutokana na hati ya mashtaka hayo kuwa na upungufu wa kisheria na waachiwe huru.

Kadhalika, mahakama hiyo imesema haina mamlaka ya kumuamuru Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) au kuwaachia huru washtakiwa kwa sababu kesi yao inasikilizwa na Mahakama Kuu.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi, baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili.

Februari 29, mwaka huu Rugemalira aliwasilisha hoja ya kumtaka DPP atoe kibali cha kumwachia huru na kwamba asipofanya hivyo mahakama hiyo imwondolee mashtaka yanayomkabili.

Mshtakiwa wa tatu, Joseph Makandege, aliwasilisha hoja zake Machi 26, mwaka huu akidai hati ya mashtaka ina upungufu wa kisheria.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kusikiliza uamuzi mdogo wa mapingamizi ya awali ya mshtakiwa wa kwanza na wa tatu.

Hakimu Shaidi alisema mahakama yake haina mamlaka ya kutekeleza hoja za washtakiwa kupitia mapingamizi yao ya awali bali wajibu wake ni kuitaja na kusoma maelezo ya mashahidi ikiwa upelelezi umekamilika na DPP kutoa kibali kwa Mahakama Kuu kuendelea kusikiliza kesi hiyo.

"Mahakama yangu imepitia hoja za mapingamizi ya washtakiwa na yote mnayoyalalamikia haina mamlaka ya kuyafanyia kazi wala kutoa amri hivyo kama mnaona kuna mambo hamridhiki nayo naomba mpeleke hoja zenu Mahakama Kuu," alisema Hakimu Shaidi.

Mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni, Harbinder Seth, ambaye aliiomba mahakama hiyo isaidie kuharakisha upelelezi wa kesi hiyo kwa kuwa umechukua muda mrefu kuanza kusikilizwa mbali na uamuzi alioufanya mwaka jana wa kuandika barua ya kukiri makosa na kuomba makubaliano na DPP bila kupata majibu.

Akijibu hoja ya Seth, hakimu Shaidi alisema hakuna mahakama inapenda kuchelewesha kesi na kuongeza kuwa kama angekuwa na mamlaka angeshaifuta.

Kuhusu barua aliyoiandika kwa DPP hakimu alisema kuwa utaratibu huo wa kisheria ni kati ya ofisi ya DPP na mshtakiwa, hivyo mahakama haihusiki kwa chochote bali inasubiri taarifa tu kutoka kwa pande hizo mbili.

Baada ya uamuzi huo kutolewa mshtakiwa Rugemalira alikubaliana na uamuzi wa kwenda Mahakama Kuu na kuomba apatiwe nakala uamuzi huo mdogo.

Hakimu alisema kesi hiyo ilitajwa Mei 21, mwaka huu na washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu.

Washtakiwa Seth na Rugemalira kwa pamoja na Joseph Makandege, wanakabiliwa na mashtaka 12 yakiwamo ya utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh. 309,461,300,158.27.

Rugemalira na Seth walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Juni 19, 2017.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live