Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rufaa ya aliyemmwagia mafuta mumewe yagonga mwamba

Dhamana, Hukumu Rufaa ya aliyemmwagia mafuta mumewe yagonga mwamba

Mon, 22 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati familia huanza mlo kwa kifungua kinywa asubuhi, kwa Lameck Anaclet haikuwa hivyo, mkewe, Jackline Josephat alichemsha mafuta ya kupikia na kummwagia mwilini.

Hili ni tukio lililotokea asubuhi ya Desemba 13, 2021 na mkewe alitoroka na kumwacha Lameck akipata msaada kutoka kwa majirani.

Hata hivyo, Jackline alikamatwa na kufikishwa kortini alikohukumiwa kifungo cha miaka mitano jela. Related

Mke apigwa na mumewe hadi kufa kwa kosa la 'kukata mauno' Kimataifa 8 min ago Mwanaume auwa wanawe wawili kisa kuachwa na mke Kimataifa 8 min ago

Baada ya hukumu, hakuridhika na adhabu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Ilemela Jijini Mwanza Januari 23, 2023, hivyo alikata rufaa Mahakama Kuu ambayo Mei 19, 2023 iliitupilia mbali rufaa hiyo.

Mrufani huyo aliegemea sababu nne, akidai Mahakama ilikosea kuegemea ushahidi wa mumewe kinyume cha sheria na kwamba tukio hilo lilitokea baada ya kukosekana amani baina yao.

Katika sababu hizo za rufaa, alieleza kuwa siku ya tukio asubuhi, mumewe alitishia kumfukuza moja kwa moja katika nyumba yao wanayoishi na sababu hiyo ililenga kuionyesha Mahakama kuwa yeye ndiye alichokozwa.

Akijenga hoja mbele ya Jaji Morris, alisema alikimbia kutoka eneo la tukio baada ya uhalifu unaodaiwa kutendwa kwa ajili ya kufuata usuluhishi na upatanishi wa dada yake na si vinginevyo.

Jackline aliieleza kuwa Mahakama ya Wilaya ya Ilemela, ilikubali na kuufanyia kazi ushahidi wa kusikia kutoka kwa shemeji yake, Erasto George aliyekuwa shahidi wa pili ambaye hakuwepo eneo la tukio.

Hata hivyo, sababu zote hizo zilipanguliwa na mawakili wa Jamhuri kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Japhet Ngussa na Sileo Mazullah na kusisitiza kuwa kutiwa kwake hatiani kulikuwa sahihi na Mahakama ilizingatia ushahidi wote.

Mawakili hao walisema Mahakama hiyo ilizingatia kuwa kitendo cha yeye kutoroka ni ushahidi wa makusudi alimmwagia mumewe mafuta.

Jaji Dk Cleophace Morris alisema uhalifu unapotendwa kwa shahidi kama huyo, anasa ya kisheria inaondolewa kwa sababu haupaswi kudhoofishwa au kupunguzwa na sifa za hisia za ndoa.

Kuhusu hoja ya kuchokozwa kwamba Mahakama haikuzingatia utetezi wake huo, Jaji alisema kumbukumbu za ushahidi wake zinaonyesha alijitetea alikuwa anakaanga pop-corn ndio mafuta yakamrukiwa mumewe.

Jaji pia alichambua hoja kuwa ushahidi wa shahidi wa pili (George) ulikuwa ni wa kuambiwa, unajibiwa na mrufaniwa (Jamhuri) kwamba mtu aliyepata majeraha anahitaji kusaidiwa na sio kukimbiwa kama ilivyo kesi hiyo.

Kwa mujibu wa ushahidi wa George, wakati anakimbilia nyumbani kwa Lameck, alikutana na Jackline akiwa kwenye bodaboda akijaribu kutoroka na alipomhoji alimjibu kuwa amemmwagia kidogo mafuta ya moto usoni.

Kuhusu utetezi wake kwamba alikuwa anakimbilia kwa dada yake kuomba msaada, Jaji Morris alisema hoja hiyo ilijibiwa vizuri na Jamhuri kuwa mtu mwenye hekima alitarajiwa kutafuta msaada kwa majirani wa Lameck.

Jaji Morris alisema rufaa hiyo imekosa mashiko hivyo kutiwa kwake hatiani ni sahihi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live