Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rufaa ya Sabaya na wenzake kuendelea leo

Sabaya Rufaa Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya

Wed, 28 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, leo imepanga kuendelea kusikiliza rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kupinga hukumu iliyomwachia huru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Wajibu rufaa wengine, mbali na Sabaya ni Enock Mnkeni, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.

Akiahirisha rufaa hiyo Desemba 21, 2022, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Judith Kamala alisema rufaa hiyo itaendelea kusikilizwa leo baada ya tangazo la hati ya wito kwa wajibu maombi wanne kutolewa kwa mara ya pili katika magazeti. Desemba 14, 2022 Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza rufaa hiyo, aliahirisha kuisikiliza na kutoa amri kwa Naibu Msajili wa Mahakama kuchapisha kwenye magazeti tangazo la hati ya wito kwa wajibu rufaa wanne kwenye rufaa hiyo ambao hawakuwepo mahakamani hapo ambao ni Mnkeni, Aweyo, Macha na Msuya.

Rufaa hiyo ilianza kusikilizwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Desemba 13 mwaka huu, ambapo mawakili wa mjibu maombi wa kwanza (Sabaya), waliwasilisha pingamizi la awali wakiomba Mahakama kutupilia mbali rufaa hiyo wakidai haiko sawa kisheria, wakitaja sababu mbili, zikiwemo kukatwa nje ya muda na notisi ya rufaa inatofautiana na maombi ya rufaa yaliyowasilishwa mahakamani hapo.

Wakijibu hoja hizo za pingamizi, mawakili wanaomwakilisha muomba rufaa waliiomba Mahakama kutupilia mbali pingamizi hilo, wakidai nyaraka zilizopo mahakamani hapo zimekidhi matakwa ya kisheria na baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili Desemba 14, 2022 Jaji huyo alitoa uamuzi mdogo wa pingamizi hilo na kueleza kuwa rufaa hiyo imewasilishwa ndani ya wakati.

Rufaa hiyo inapinga hukumu iliyotolewa Juni 10, 2022 na Hakimu Mkazi, Patricia Kisinda wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, iliyowaachia Sabaya na wenzake sita waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Chanzo: Mwananchi