Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rufaa mbili za Zumaridi zarindima Mahakama Kuu

Picha Zumaridi Data Rufaa mbili za Zumaridi zarindima Mahakama Kuu

Fri, 28 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rufaa mbili tofauti zimeanza kuunguruma mbele ya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kuhusu hukumu ya kifungo cha miezi 12 aliyopewa Diana Bundala maarufu kama "Mfalme Zumaridi" baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuzuia maofisa wa Serikali kutekeleza majukumu yao.

Wakati upande wa Jamhuri umekata rufaa kupinga adhabu hiyo kuwa ndogo kwa mujibu wa sheria, upande wa ‘Zumaridi’ nao umekata rufaa kupinga adhabu hiyo ukidai haikustahili kutolewa.

Rufaa hizo zilizosajiliwa kwa namba 72/2023 (upande wa Zumaridi) na namba 32/2023 iliyowasilishwa na Jamhuri zimesikilizwa leo Alhamisi Julai 27, 2023, mbele ya Jaji Cleoface Morris kwa pande zote kutoa hoja zao za rufaa.

Akiwasilisha hoja za rufaa kwa upande wa Jamhuri, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Dorcas Akyoo akisaidiana na Frank Nchanila na Adam Murusuli wameiomba Mahakama kumuongezea adhabu Zumaridi na wenzake wanne waliotiwa hatiani kwa madai kuwa adhabu waliyopewa awali ilikuwa ndogo kwa mujibu wa sheria.

Pamoja na kuwasilisha hoja za rufaa, Wakili Dorcas pia ameiomba Mahakama kutupilia mbali rufaa iliyowasilishwa na upande wa Zumaridi akidai notisi ya rufaa ilichelewa kuwasilishwa.

"Notisi ya mrufani iliwasilishwa Februari 6, 2023, ikiwa ni siku 13 baada ya hukumu badala ya muda wa kisheria wa siku 10 kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai Sura ya 20 mapitio ya mwaka 2022,’’ amedai Wakili Dorcas

Hata hivyo, hoja hiyo imepingwa na upande wa Zumaridi kupitia kwa Wakili Erick Mutta akisema kifungu cha sheria kilichotajwa na upande wa Jamhuri hakitoshi kuifanya rufaa yao kutupwa.

Kuhusu hoja za rufaa, Wakili Mutta ameiambia Mahakama kuwa adhabu dhidi ya wateja wake ilikuwa kubwa kulinganisha na makosa yao, hivyo kuiomba Mahakama kutengua hukumu ya awali iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza.

Katika hukumu yake ya Januari 25, 2023, katika shauri la jinai namba 10/2022, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, Monica Ndyekobora alimtia hatiani Zumaridi na wenzake wanne na kuwahukumu kifungo cha miezi 12 jela kwa kosa la kuwazuia maofisa wa Serikali kutekeleza majukumu yao.

Zumaridi wa wenzake walidaiwa kumzuia Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Nyamagana, Christina Mwisongo (46) na maofisa wa Jeshi la Polisi kutekeleza majukumu yao walipofika kwenye makazi yake eneo la Buguku jijini Mwanza.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji Morris ameahirisha shauri hilo hadi Agosti Mosi, 2023 atakapotoa maamuzi huku akisema iwapo rufaa zote zitakubalika; basi zitasikilizwa kwa pamoja.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live