Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rufaa dhidi ya Gekul yaiva, hukumu Aprili 15

GEKUL11 1 Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul.

Fri, 5 Apr 2024 Chanzo: Mwananchi

Mbivu au mbichi zitajulikana Aprili 15, 2024, Mahakama itakaposoma hukumu ya rufaa ya jinai iliyofunguliwa na Hashim Ally dhidi ya Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul.

Awali, Hashim alimfungulia kesi ya jinai katika Mahakama ya Wilaya ya Babati, Gekul aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, akimtuhumu kumfanyia shambulio la kudhuru mwili analodai lilitendwa Novemba 11, 2023.

Desemba 27, 2023, Hakimu Victor Kimario aliifuta kesi hiyo kutokana na uamuzi wa DPP kwa kutumia kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) Sura ya 20 kama kilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

Hata hivyo, Hashim anayewakilishwa mahakamani na Wakili Peter Madeleka, alikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, akidai hajaridhishwa na amri ya kuifuta kesi iliyotolewa na Hakimu Kimario, akijenga hoja tano.

Hoja ya kwanza ni kwamba, hakimu alikosea katika sheria na ukweli kwa kushindwa kuzingatia matakwa ya sheria chini ya Ibara ya 13(6) (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Tanzania ambayo inatoa haki ya msingi ya kusikilizwa na kupata haki.

Ibara hiyo inasema: “Wakati haki na wajibu wa mtu yeyote vinahitaji kufanyiwa uamuzi wa Mahakama au chombo kingine kinachohusika, basi mtu huyo atakuwa na haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kwa ukamilifu.” Na ikaongeza kuwa:

“Na pia haki ya kukata rufaa au kupata nafuu nyingine ya kisheria kutokana na maamuzi ya Mahakama au chombo kingine kinachohusika.”

Katika hoja ya pili, mrufani anadai hakimu alikosea kisheria kwa kushindwa kuzingatia matakwa ya kisheria chini ya ibara ya 59B (4)(a),(b),(c) na (5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyofanyiwa marekebisho.

Hashim kupitia kwa Madeleka, katika hoja ya tatu analalamika kuwa hakimu alifanya makosa makubwa ya kisheria pale aliposhindwa kuzingatia kifungu cha 228(1) cha CPA kama kilivyorekebishwa mwaka 2022.

Katika hoja ya nne, mrufani anadai hakimu alikosea kisheria na katika ukweli, baada ya kushindwa kuzingatia ukweli kuwa wakati anatoa amri ya kuifuta kesi hiyo, mshtakiwa katika kesi hiyo (Pauline Gekul) hakuwepo mahakamani.

Hoja ya tano, anadai hakimu alikosea kisheria pale amri yake ilipoegemea taarifa ya DPP ya Nolle Prosequi ambayo haikuwasilishwa sawasawa mahakamani, na hoja ya sita ni kuwa hakimu alizingatia Nolle Prosequi iliyopelekwa kortini bila kuzingatia sheria.

Mapingamizi ya awali

Machi 21, 2024 Jaji Devotha Kamuzora, alisikiliza kwa mara ya kwanza rufaa hiyo sambamba na pingamizi la awali lililoibuliwa na mrufaniwa (Gekul), siku moja kabla, Machi 20, akipinga rufaa hiyo kusikilizwa, huku akiwasilisha hoja tatu.

Gekul kupitia wakili wake, Ephraim Kisanga, katika hoja ya kwanza anadai Mahakama haikuwa na uwezo wa kusikiliza rufaa hiyo kwa kuwa sababu ya kwanza na ya pili ya rufaa ilikuwa imehusisha hoja zinazohusu Katiba na kwa maana hiyo, Mahakama hiyo haikuwa ya kikatiba.

Sababu ya pili anadai rufaa hiyo imewasilishwa mapema kabla ya wakati, hivyo haistahili kusikilizwa; na sababu ya tatu anadai kesi haipaswi kuzingatiwa kwa ujumla.

Mrufani kupitia mawakili watatu wakiongozwa na Madeleka, walidai mapingamizi hayo hayakuwa na mashiko na kusisitiza Mahakama ina mamlaka ya kisheria kupokea rufaa zote zinazotokana na maamuzi ya Mahakama za chini.

“Kusema kwamba haina mamlaka ni upungufu wa usahihi na hoja nyingine ni kwamba, DPP hakuwa sehemu ya kesi, hivyo hakuwa na mamlaka na haki ya kuingilia kesi ile kwa namna ambavyo aliingilia,” alidai wakili Madeleka na kuongeza:

“Kwa sababu hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka haikuingizwa mahakamani kwa njia zinazoelekezwa na sheria.”

Baada ya kusikiliza pingamizi, Jaji alisema uamuzi atautoa pamoja na hukumu ya rufaa hiyo.

Baada ya kukamilika usikilizwaji wa hoja za pande mbili, Jaji Kamuzora alipanga kutoa hukumu Aprili 15, 2024 saa 8.00 mchana.

Wakili Madeleka amelithibitishia gazeti hili kupokea wito huo wa Mahakama na yeye na mteja wake wako tayari kupokea uamuzi.

Tuhuma zilivyokuwa

Kwa mujibu wa hati ya malalamiko ya kesi hiyo, mbunge huyo alikuwa akikabiliwa na shtaka moja la shambulio na kusababisha madhara kwa mwili chini ya kifungu cha 241 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marekebisho ya mwaka 2022.

Gekul anadaiwa yeye na watu wengine ambao hawawepo mahakamani Novemba 11, 2023, mjini Babati, walimuita Hashim na kumuweka kizuizini, huku wakimtishia kwa silaha ya moto.

Kisha walimvua nguo na kumshambulia kwa kumlazimisha kukalia chupa ya soda ili iingie katika njia ya haja kubwa.

DPP aliwasilisha taarifa ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi hiyo chini ya kifungu cha 91(1) cha CPA, kinachompa mamlaka ya kufuta kesi yoyote ya jinai katika hatua yoyote kabla ya hukumu ya Mahakama na bila kulazimika kutoa sababu za uamuzi huo.

Chanzo: Mwananchi