Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ripoti ya anayedaiwa kuuawa na polisi hadharani

Mon, 3 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tabora. Uchunguzi wa mwili wa mfanyabiashara wa nyama mjini Igunga mkoani Tabora, Seleman Jumapili (22) anayedaiwa kuuawa na polisi unaonyesha kifo chake kimetokana na kupigwa na kitu kizito kichwani.

Mganga mkuu wa mkoa wa Tabora, Dk Gunini Kamba na mganga mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Kitete, Dk Kelvin Nyakimori walioufanyia uchunguzi mwili huo, walieleza kuwa uchunguzi unaonyesha kuwa kifo chake kilitokana na kupigwa na kitu kizito kisogoni.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri aliyesimamia uchunguzi na maziko ya mfanyabiashara huyo juzi, aliwataka wananchi wa Igunga kuwa watulivu wakati suala hilo likishughulikiwa na vyombo vya dola.

Alimuagiza kamanda wa polisi mkoa huo, Emmanuel Nley kuwakamata askari wote wanaotuhumiwa kuhusika.

Mwanri alisema Serikali haiwezi kuvumilia kuona baadhi ya watu wakichafua sifa yake nzuri ya kufanya kazi kwa weledi na kuwatumia wananchi hasa wanyonge.

Akizungumzia tukio hilo, Nley alisema hadi sasa polisi tisa wanashikiliwa ila hakuwa tayari kuwataja kwa sababu uchunguzi unaendelea.

Naye mbunge wa Igunga, Dk Dalaly Kafumu ambaye ni miongoni mwa viongozi walioshiriki mazishi ya kijana huyo yaliyofanyika katika makaburi ya Masanga, alilaani vikali kitendo hicho na kuwataka askari kufanya kazi kwa kuzingatia sheria za nchi.

Kafumu alimuomba Mwanri kufuatilia suala hilo kwa karibu ili haki siyo tu itendeke, bali ionekane inatendeka.

Polisi wanadaiwa kumuua Seleman mkazi wa mtaa wa Mwayunge mjini Igunga, inaelezwa walimkamata kazini kwake na kumpiga hadi kulazwa hospitali.

Naye mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya Igunga, Dk Merchades Magongo alikiri kumpokea Selemani saa 3:00 usiku ya Agosti 29 akiwa na polisi na kwamba, wakati akiendelea kumhudumia saa tano usiku alifariki.

Chanzo: mwananchi.co.tz