Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ripoti Maalum: Shambulio mishale dhidi ya walimu lazua taharuki

MSHALE Ripoti Maalum: Shambulio mishale dhidi ya walimu lazua taharuki

Fri, 26 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

*Mmoja auawa, mwingine ajeruhiwa

WALIMU katika Kijiji cha Chihwanga, Kata ya Itaragwe wilayani Gairo mkoani Morogoro, wamejikuta katika taharuki kutokana na mfululizo wa matukio ya mashambulizi dhidi yao kwa kutumia mishale yaliyosababisha kifo cha mmoja wao.

Kijiji hicho kiko umbali wa kilometa 40 kutoka mjini Gairo, na hadi sasa mwalimu mmoja ameuawa kwa kile kilichodaiwa wivu wa mapenzi na mmoja kujeruhiwa kutokana na kile kinachohusishwa na ushahidi alioutoa kwa vyombo vya dola kuhusu tukio la kushambuliwa kwa mwalimu mwenzake.

Kutokana na matukio ya kushambuliwa kwa walimu, baadhi ya wawezeshaji hao wa taaluma kwa wanafunzi wameomba kuhamishwa kituo cha kazi, lakini hadi sasa hawajafanikiwa.

Matukio hayo yalitokea mwishoni mwa Februari mwaka huu kwa mwalimu wa kwanza kuchomwa mshale na Juni 20 mwaka huu, mwalimu mwingine alipochomwa mshale katika eneo la uwanja wa shule ya msingi, karibu na eneo alikouawa mwalimu wa kwanza na sasa majeruhi huyo amelazwa Kituo cha Afya Gairo.

Nipashe ilizuru katika kijiji hicho na kumtembelea kituo cha afya Mwalimu Hosea Kikoye wa Shule ya Sekondari Iyogwe, ambaye ana majeraha kwenye mkono wa kushoto.

Akisimulia tukio hilo, mwalimu huyo alisema lilitokea Juni 20 mwaka huu, majira ya saa tatu usiku, kwenye uwanja wa mpira wa shule, jirani kidogo na nyumba anayoishi ambazo ni za shule, wakati akitoka kwenye shughuli zake (ana duka) jirani na eneo hilo.

"Nilivamiwa na watu ambao siwafahamu, nilishangaa tu nikiwa njiani namulikwa na mwanga baadaye ukazimwa. Nilishtuka nikapigwa mshale wa mkono.

"Ninafikiri lengo lao lilikuwa wanipige kifuani, Mungu alinisaidia, nilipiga kelele walijitokeza baadhi ya walimu na wanakijiji wema wakanipeleka kupata huduma ya kwanza," Mwalimu Kikoye alisimulia.

Mwalimu huyo alilihusisha tukio la kushambuliwa kwake na ushahidi alioutoa polisi kuhusu mauaji ya mwalimu mwenzake, Madaraka Mwanilwa, aliyeuawa kwa kuvamiwa na watu wasiojulikana na kuchomwa mshale shingoni Februari 24 mwaka huu kwenye uwanja huo huo.

“Hii ni mara ya pili, ninadhani lengo lao kubwa ni kufuta ushahidi, baada ya awali kumsaidia mwalimu mwenzangu aliyepigwa mkuki na mimi kumsaidia, lakini baadaye akafariki, niliitwa polisi kuhojiwa maswali mbalimbali kuhusu kifo chake na nilieleza kila kitu nilichoelezwa na marehemu kabla hajafariki dunia,” alisema.

Aliendelea kusimulia kuwa kufuatia tukio la kuuawa kwa mwalimu huyo, baadhi ya watu walikamatwa na kufikishwa mahakamani na baadaye kesi ilihamishiwa mjini Morogoro.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Gairo, Dk. Bonithe Calist, aliyempokea majeruhi huyo, akizungumza na Nipashe, alisema majeruhi huyo alifikishwa hospitali akiwa na maumivu makali na mshtuko.

Kuhusu mshale aliochomwa kuwa na sumu au la, Dk. Calist alisema kitaalamu siyo rahisi sana kugundua kwa haraka, lakini jitihada zimefanyika ili sumu isisambae mwilini.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Iyogwe, Maria Mdoe, alithibitisha kutokea kwa matukio hayo na kusema kuwa ni mfululizo wa matukio yenye kuzua taharuki kwa watumishi wa kada hiyo.

Alisema matukio hayo yanashusha morali ya kazi kwa shule ambayo imeshika nafasi ya pili kiwilaya kwenye matokeo ya kidato cha nne mwaka jana, kwa kuwa walimu sasa wanaishi kwa hofu ya maisha yao.

“Tukio hili linatukumbusha la Mwalimu Madaraka Mwanilwa, hatujui ni vuguvugu la kitu gani lilikuwa linaendelea bila sisi kufahamu hadi mwalimu mwingine Hosea Charles alipopigwa mshale,” alisema.

Kwa mujibu wa mwalimu huyo, Mwanilwa aliwahi kuomba kuhamishwa kituo tangu Oktoba mwaka jana baada ya kuwa amefundisha kwenye shule hiyo kwa zaidi ya miaka 10, lakini hadi sasa, taratibu za ngazi za juu hazijakamilika.

“Ninaiomba serikali iliangalie suala hili, huenda itaondoa matatizo kama haya yaliyojitokeza ya kifo na taharuki kwa walimu. Kwa mazingira ya namna hii ambayo walimu wanawindwa kama swala, hatuwezi kuvumilia ndiyo maana tunaomba serikali itusaidie,” alisema.

Kwa mujibu wa mkuu wa shule huyo, mwalimu aliyeuawa na kuzikwa mkoani Iringa, alichukiwa kijijini kwa vile ni msomi na mchapakazi, na hata akijichanganya na wanakijiji alikuwa anatengwa kwa madai kuwa ana majivuno.

“Tunadhani ilikuwa ni sababu ya wao kumwinda na kumuua, na huyu wa pili aliyejeruhiwa inaonekana walisikitika kwa kuona kwanini walimu hawa walisaidiana, na kwanini walipohojiwa polisi walitaja baadhi ya wanakijiji.

“Ni kweli walimu wengine karibu wanne wanatajwatajwa kulipiziwa kisasi kwa sababu kama hizo, walimu wote waliopo hapa siyo wazawa wa Mkoa wa Morogoro, lakini jamii inapaswa kuelimishwa kuwa kila Mtanzania ana sifa ya kuishi popote bila kuvunja sheria.

“Kutokana na hizi taarifa zinazoendelea zinazofanywa walimu wasijiamini, hata kitaaluma shule haitakaa vizuri sana, ingawa mwaka jana tulikuwa wa pili kiwilaya.

"Walimu sasa wamevunjika moyo na kukata tamaa kabisa kutokana na matukio haya kuwa ya mfululizo na ya aina ileile,” mkuu wa shule huyo alilalamika.

Mwalimu huyo anasema shule ilikuwa na walimu 24, lakini wengi walihama kutokana na matatizo mbalimbali.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, akifafanua: “Alichomwa mshale na mtu asiyejulikana, akakimbilia kwa walimu wenzake na wakamsaidia kumpeleka Zahanati ya Iyogwe na baadaye kuhamishiwa Kituo cha Afya Gairo kwa matibabu zaidi baada ya kuonekana anavuja damu nyingi.

"Sasa hali yake inaendelea vizuri na sisi tunaendelea kuchunguza tukio hili na waliohusika."

Kamanda Mutafungwa pia alithibitisha kuuawa kwa mwalimu katika shambulio la Februari, wahusika wakitumia mishale na chanzo kikidaiwa kuwa wivu wa kimapenzi.

Alibainisha kuwa watuhumiwa wawili wa tukio hilo la kwanza walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani humo wakikabiliwa na kesi namba 34/2020.

Mmoja wa wakazi wa Gairo, Jeremiah Mwegoha, alisema alishuhudia baadhi ya wanakijiji wakikamatwa na Jeshi la Polisi baada ya kutokea kwa tukio la kwanza.

Aliiomba serikali na vyombo vya usalama kufuatilia kwa kina suala hilo, ili kuondoa taharuki hiyo na kurejesha uhusiano mwema baina ya pande zote.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kijiji hicho, Andrea Majosti, alisema mara kwa mara wanaelimisha jamii kuhusu mambo mbalimbali na hakuna ugomvi baina ya kijiji na shule hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe, akiiongoza kamati yake ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya akiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Agness Mkandya, na maofisa wengine katika halmashauri hiyo, walizuru kijijini huko Jumanne na kuzungumza na wananchi na walimu katika mikutano tofauti.

Eneo hilo la Iyogwe limekuwa likidaiwa kuwa na dosari ya kuwekwa masharti magumu kwa watu wageni wanaoingia huko kwa lengo la kuweka makazi.

Kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo waliozungumza na Nipashe, baadhi ya masharti kwa wageni kaya kutakiwa kuchota maji ndoo moja pekee kwa siku kwa matumizi mbalimbali, kuzuiwa kutwanga chochote kuanzia saa 12 jioni ili kukidhi mila na desturi zilizoelezwa ni za Kikaguru ambao ndiyo wenyeji wa eneo hilo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live