Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu raia wa Rwanda, Fatuma Kalufan (31) kutumikia kifungo cha miaka miwili jela kwa kosa la kuingia na kuishi Tanzania bila kibali.
Pia, mahakama hiyo imesema mshtakiwa baada ya kumtumikia kifungo hicho arejeshwe nchini kwao.
Hukumu hiyo imetolewa leo Alhamisi Novemba 11, 2021 na Hakimu Mkazi Mkuu, Ritha Tarimo amesema mshtakiwa huyo amekuwa akifanya makosa hayo mara kwa mara.
Tarimo ameieleza mahakama hiyo kuwa hukumu hiyo ni ya mara ya pili kutolewa kwa mtuhumiwa huyo.
“Katika kesi ya namba CC 229/2015 mshtakiwa alihukumiwa mbele ya hakimu Tespicious Mwijage kwenda jela miaka miwili au kulipa faini kwa kosa la kusema ni raia wa Uganda badala ya kusema ni raia wa Rwanda lakini alilipa faini na kisha kurudishwa nchini kwao.” Hakimu Tarimo
Amesema mwaka 2018 mshtakiwa huyo akiwa raia wa Rwanda aliingia na kuishi nchini bila kibali na alifunguliwa kesi katika mahakama hiyo namba CC 285/2018 ambapo alihukumiwa kulipa faini mbele ya hakimu, Wanja Hamza na kisha kurudishwa nchini kwao.
“Mwaka 2021 mshtakiwa huyo alishtakiwa mahakamani hapa kwa makosa haya haya hivyo mahakama inamuhukumu kutumikia kifungo cha miaka miwili jela na atakapomaliza adhabu hiyo arejeshwe chini kwao” ” amesema Tarimo
Awali wakili wa Serikali, Shija Sitta aliieleza mahakama hiyo kuwa mshtakiwa amekuwa akiichezea serikali hivyo aliomba apewe adhabu kali ya bila faini ili we fundisho kwa watu wenye tabia kama hiyo.