Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Raia wa Msumbiji kwenda jela au kulipa faini Sh883.5 milioni

Hukumu Pc Data Raia wa Msumbiji kwenda jela au kulipa faini Sh883.5 milioni

Wed, 13 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, imemhukumu kifungo cha miaka 20 jela au kulipa faini ya Sh883.5 milioni raia wa Msumbiji Armelindo Anibal (43) kwa kosa la kukutwa na pembe mbili za faru zenye thamani ya Sh88.3 milioni.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Charles Mzava, ametoa hukumu hiyo leo Septemba 13, 2023; mara baada ya kusikiliza hoja za pande mbili za mashtaka na utetezi.

Amesema ametoa adhabu hiyo kwa kuzingatia kwamba mnyama faru ni miongoni mwa wanaopotea na wanaoliingizia Taifa fedha za kigeni kupitia sekta ya utalii.

"Hivyo basi kwa kuzingatia thamani ya mnyama adhabu yake inapaswa kuwa kubwa na kwa mujibu wa sheria ya wanyama pori sura ya 283,” amesema Hakimu Mzava.

Kwa mujibu wa hakimu huyo, kifungu hicho kinasema: “Mtu yeyote atakayekutwa na nyara za serikali zenye thamani zaidi ya Sh100, 000 atapigwa faini zaidi ya mara kumi ya thamani ya hiyo nyara, au ataenda jela si chini ya miaka 20 na sio zaidi ya miaka 30.”

Katika utetezi wake, Wakili wa mshtakiwa, Alex Msalenge, aliiomba mahakama kumpa mteja wake adhabu ndogo kwa kuwa pamoja na mambo mengine, kwanza hakuwa na lengo la kufanya uhalifu, pili tayari alishakaa ndani muda mrefu, umri wake ni mkubwa hivyo Taifa lake na wategemezi wanamuhitaji, na kwamba ni mgeni hivyo hakujua kama anatenda kosa.

Armelindo alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Desemba 7, 2021 baada ya kukamatwa wilayani Masasi baada ya jeshi la polisi kupewa taarifa na raia wema juu ya kuwepo na mtu asiyejua kiswahili na mzigo usioeleweka kwenye gari.

Hata hivyo Hakimu Mnzava amesema anakubaliana na hoja nyingine lakini suala la ugeni wake halikumpa haki mtuhumiwa kukiuka sheria za nchi.

Wakili wa Serikali, Alex Kasela aliiiomba Mahakama hiyo kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwake na raia wengine wa kigeni na wanaodhani kwamba Tanzania ni nchi ya kufanya biashara haramu.

Wakili Alex alisisitiza kuwa adhabu kali itolewe kwa vile mnyama aliyeuwawa ni miongoni mwa wanyama adimu hivyo ameharibu uchumi wa nchi.

Kesi hiyo pia iliendeshwa na mawakili wa serikali, Atuganile Nsajigwa na Florence Mbamba

Chanzo: www.tanzaniaweb.live