Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Raia wa Burundi jela kwa kuishi nchini kinyume cha sheria

Ceo D . Law Raia wa Burundi jela kwa kuishi nchini kinyume cha sheria

Tue, 21 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu raia watano wa Burundi kila mmoja kulipa faini ya Sh1 milioni au kwenda jela mwaka mmoja, baada ya kupatikana na hatia katika makosa mawili ambayo ni kuingia na kuishi nchini bila ya kuwa na kibali.

Washtakiwa hao, ambao ni wauza kahawa eneo la Jangwani na Mchikichini, wamehukumiwa kulipa faini hiyo, Februari 20, 2023 baada ya kukiri mashtaka yao.

Waliohukumiwa kulipa faini hiyo ni Jephason Jerald (38), Michael Bahati (28), Kalenzo Kabatari (31), Abdallah Masumbuko (25) na Nimubona Jastin (23).

Wakati washtakiwa hao watano wakikiri mashtaka yao, mshtakiwa wa sita katika kesi hiyo ya jinai namba 33/2023 mshitakiwa Novatus Buzwili, amekana mashtaka yanayomkabili.

Hata hivyo, washtakiwa hao wameshindwa kulipa faini na hivyo watatumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani.

Akisoma hukumu hiyo, Februari 20, Hakimu Mkazi Mkuu, Amir Msumi amesema washtakiwa wametiwa hatiani kama alivyoshtakiwa.

Hakimu Msumi amesema amezingatia kuwa washtakiwa wote ni wakosaji kwa mara ya kwanza na upande wa mashtaka hauna kumbukumbu zozote za nyuma za makosa ya jinai waliyofanya.

"Pia Mahakama hii imeangalia umri wenu, bado mnatakiwa kuzalishaa mali na kuijenga nchi na nimezingatia pia mnategeme na familia zenu, hivyo nimesukumwa kuwapa adhabu ya kila mmoja kulipa faini ya Sh500,000 kwa kila kosa na mtu akishindwa anatakiwa kutumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani na kwamba adhabu hii inakwenda kwa pamoja," amesema Hakimu Msumi

Awali, kabla ya kutoa adhabu hiyo, Hakimu Msumi aliwahoji washtakiwa sababu za wao kuingia na kuishi nchini bila kuwa na kibali na kwa nini asipewe adhabu kali.

Washtakiwa hao waliomba msamaha na kuomba Mahakama iwapunguziwe adhabu kwa kuwa wanafamikia wameziacha nchini Burundi ambazo zinawategemea na ni kosa lao la kwanza.

Hata hivyo, kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, kutoka Idara ya Uhamiaji, Godfrey Ngwijo akisaidiana na Shija Sitta, waliomba mahakama itoe adhabu kali dhidi washtakiwa hao ili iwe fundisho kwa wenzao.

"Tunaiomba mahakama itoa adhabu kali kwa washtakiwa hawa kwa sababu nchi wanayotoka ni mwanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki( EAC), hivyo hawahitaji kuwa na viza bali wamefanya makusudi tu, kwa kushindwa kufuata utaratibu uliopo ili waweze kuingia nchini," amesema wakili Ngwijo.

Kwa upande wake mshtakiwa Buzwili, yeye amerudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti dhamana, ambayo ni Mahakama ilimtaka awe na wadhamini wawili na mmoja wapo asaini fedha taslimu Sh8 milioni huku mwingine asaini bondi ya Sh500, 000.

Mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana na hivyo kurudishwa rumande hadi Februari 27, 2023, ambapo kesi yake itaitwa kwa ajili ya kusomewa hoja za awali (PH).

Katika shtaka la pili, siku na eneo hilo, washtakiwa wanadaiwa kuishi nchini kinyume cha sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live