Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC atuhumu Polisi kumiliki mitambo ya gongo

E7f0c7a398d74f8e4b854dfa9b9062ea.png RC atuhumu Polisi kumiliki mitambo ya gongo

Thu, 25 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, amewatuhumu baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi kwa wao kumiliki mitambo ya kutengenezea pombe haramu ya gongo.

Pia aliwatuhumu baadhi ya Polisi kuwa wanamiliki vyombo vya moto ambavyo vimekuwa chanzo cha uvunjifu wa sheria za barabarani na kusababisha malalamiko kwa wananchi.

Mghwira alitoa tuhuma hizo jana mjini Moshi katika kikao cha kusikilizia kero za wafanyabiashara kilichoandaliwa na ofisi yake na akasema, Polisi hao wamekuwa wakijihusisha na biashara ya gongo jambo ambalo halikubaliki.

"Mkuu wa Wilaya ya Rombo ametusaidia sana, tulikamata gongo nyingi sana huko na mitambo na wamiliki wakubwa ni askari Polisi na wananchi ni watengenezaji tu kwa hiyo ukamataji ulishindikana na hata kuna siku tulikaa kikao hapa kabla ya kutoka mitambo ikawa imefichwa"alisema.

Alisema, askari Polisi wamekuwa wakichochea vitendo vya uhalifu kinyume kabisa na maadili ya kazi na kwamba katika suala la uvunjifu wa sheria za barabarani vyombo vya moto wanavyovimiliki vimekuwa vikiongoza.

Wakati huo huo Mghwira aliagiza baa zote mkoani humo zifungwe saa 5:00 usiku kwa siku za kazi na saa 6:00 usiku kwa siku za mwishoni mwa wiki.

Alisema kwa siku za kazi baa zote zifunguliwe saa 10:00 jioni na akaagiza wafanyakazi wote watakaofika kazini asubuhi wakiwa wamechoshwa na ulevi (hangover) wachukuliwe hatua.

Chanzo: habarileo.co.tz