Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Singida aagiza TAKUKURU kuhakikisha rushwa ya ngono inakomeshwa

RC Singida Aagiza TAKUKURU Kuhakikisha Rushwa Ya Ngono Inakomeshwa RC Singida aagiza TAKUKURU kuhakikisha rushwa ya ngono inakomeshwa

Tue, 2 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) kushirikiana na vyama vya wafanyakazi kuhakikisha vitendo vya rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kijinsia vinakomeshwa mkoani hapa.

Serukamba ambaye alikuwa mgeni rasmi ameyasema hayo leo kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Uwanja wa Liti mkoani hapa.

“Vitendo vya rushwa ya ngono maeneo ya kazi na mashuleni vimekuwa vikisikika mara kwa mara nawaomba Takukuru na vyama vya wafanyakazi hakikisheni muna vikomesha,” alisema Serukamba.

Aidha, Serukamba amevisisitiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha vinaendelea na jitihada za kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama inabaki kuwa shwari ndani ya Mkoa wa Singida.

Alikadhalika Serukamba ameitaka Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wa NSSF na PSSSF kuhakikisha inawalipa mafao ya wastafu kila mwaka badala ya kuchelewesha malipo hivyo kuleta hadha kwao ya kufuatilia mafao yao.

Pia Serukamba alisema Serikali inatambua mchango wa vyama vya wafanyakazi vilivyo chini ya Shirikisho la vyama hivyo (TUCTA) na jitihada vinavyofanya katika kutetea haki na maslahi ya wafanyakazi.

Mwenyekiti wa TUCTA Mkoa wa Singida, Agnes John akizungumza wakati akitoa taarifa ya chama hicho ameiomba Serikali kuwalipa mishahara bora ambayo itakidhi mahitaji ya msingi ya binadamu ikiwemo kupewa ajira yenye staha.

Agnes alisema mshahara bora unawawezesha wafanyakazi kupata mahitaji yao ya msingi ikiwemo kuweka akiba kwa ajili ya kusomesha watoto wao na kusaidia katika mambo mengine muhimu ya kimaendeleo.

Alisema kutokana na kulipwa mishahara duni baadhi ya wafanyakazi wamekuwa na changamoto mbalimbali na kushindwa kuyamudu maisha yao ya kila siku.

Akizungumzia ajira yenye staha Agnes alisema kumekuwa na tabia kwa baadhi ya viongozi na wanasiasa kuwaweka mahabusu watumishi wa umma pale wanapobainika kukiuka taratibu za utendaji kazi jambo ambalo ni udhalilishaji mkubwa kwa wafanyakazi hao.

Agnes alitumia nafasi hiyo kuwaomba watumishi wote mkoani hapa kufanya kazi kwa bidii na kutunza vifaa vilivyoletwa na Serikali baada ya kukamilisha miradi ya maendeleo kama ujenzi wa vituo vya Afya, Hospitali, Shule na Maabara.

Mratibu wa TUCTA Mkoa wa Singida, Maria Bange alitaja baadhi ya mafanikio waliyoyapata katika kipindi cha mwaka 2022/ 2023 kuwa ni waajiri kutoa fursa kwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi kutimiza majukumu yao pasipo kubughudhiwa, ushirikiano mzuri wa vyama vya wafanyakazi na waajiri hasa wakurugenzi katika halmashauri na kuendelea kuwa na amani katika nchi yetu kumezidi kuchochea ufanisi kazini maana wafanyakazi hufanya kazi bila ya hofu.

Bange alitaja mafanikio mengine kuwa ni kupungua kwa rushwa ya ngono katika harakati za kutafuta ajira, baadhi ya waajiri kutoa fursa kwa wafanyakazi kujiendeleza kimasomo, watumishi wa Serikali kupandishwa madaraja kwa waliokuwa wanastahili, watendaji wa kata kupata posho ya mwezi, waajiri kuitisha vikao vya mabaraza ya wafanyakazi, kupunguzwa kodi katika mishahara ya watumishi na kuongezwa kwa umri (miaka) ya wategemezi katika kuhudumiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Aidha, Bange alitaja changamoto kadhaa kuwa nyongeza ya mishahara iliyofanyika mwaka jana haikukidhi matarajio ya wafanyakazi, shirika la bima kutowalipa watumishi waliokata bima ya maisha pindi bima zao zinapoiva, hivyo kupelekea malalamiko mengi kwa watumishi waliojiunga na bima hiyo.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni ucheleweshwaji pensheni kwa wastaafu, madai ya wafanyakazi juu ya fedha za uhamisho, likizo pamoja na malimbikizo ya mishahara kucheweshwa hadi wengine kustaafu.

Katika maadhimisho hayo wafanyakazi na waajiri bora walitunukiwa, vyeti, luninga na fedha taslim na vyama vyao vya kazi kama motisha kwao zawadi zilizokabidhiwa na mkuu wa mkoa ambaye alikuwa mgeni rasmi huku maadhimisho hayo yakipambwa na kunogeshwa kwa burudani mbalimbali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live