Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Kilimanjaro ashinda shauri dhidi ya wananchi KIA

Hukumu Pc Data RC Kilimanjaro ashinda shauri dhidi ya wananchi KIA

Fri, 16 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu imeyakataa maombi ya wananchi wa vijiji vinane waliokuwa wanapinga amri ya mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro kutangaza eneo lenye ukubwa wa hekta 11,000 kuwa mali ya Serikali kupitia Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA).

Hukumu ya maombi namba 2 ya mwaka 2023 imetolewa Februari 14, 2024 na Jaji Adrian Kilimi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi na nakala yake kupatikana katika tovuti ya mahakama jana, Februari 15, 2024. Kila upande utabeba gharama za kesi.

Wananchi hao kutoka vijiji vinane vya wilaya za Meru mkoani Arusha na Hai mkoani Kilimanjaro, walifungua maombi dhidi ya mkuu wa mkoa kwa cheo chake kama mdaiwa wa kwanza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama mdaiwa wa pili.

Kupitia kwa wakili wao, Jeremiah Mjema, wananchi kutoka vijiji vya Sanya Station, Mtakuja, Tindigani, Chemka, Samaria, Malula, Majengo na Kaloleni, aliiomba mahakama itoe amri ya kufuta agizo la RC Kilimanjaro, kuwa eneo lenye mgogoro ni mali ya KIA.

Walikuwa wanadai agizo la RC alilolitoa Novemba 2, 2022 lilikuwa kinyume cha sheria, lisilo na mantiki, lisilo na sababu na linakiuka haki ya asili inayotoa haki ya kusikilizwa na lilikiuka kanuni na taratibu za nchi.

Mbali na ombi hilo, walikuwa wanaiomba mahakama itoe amri dhidi ya RC ya kumzuia kuwaondoa kwa nguvu eneo hilo, kutowabugudhi na kuwatisha waombaji kutoka vijiji hivyo, pia mahakama iwape nafuu yoyote kadri itakavyoona inafaa.

Nini walichokuwa wanakilalamikia

Katika hukumu hiyo, Jaji amesema wananchi hao ni miongoni mwa wanaoishi katika eneo hilo wanaodai Novemba 2, 2022 walimsikia RC Kilimanjaro kupitia vyombo vya habari akitangaza eneo hilo walilodai ni lao la asili ni mali ya KIA.

Walidai tamko hilo la RC limeathiri vijiji vinane vilivyopo katika eneo lenye ukubwa wa hekta 11,000 katika wilaya za Meru na Hai na kwamba, wananchi hao wamejenga makazi ya kudumu na wanalitegemea kwa malisho na maisha mengine ya kitamaduni.

Kulingana na madai yao, tamko la RC la kuchukua eneo lao la asili, lilitolewa kinyume cha sheria kwa kuwa RC hakuwa na mamlaka ya kutangaza eneo lao la vijiji kuwa sehemu ya eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Walidai RC alishafanya uamuzi ndiyo maana maofisa wake wameanza kuweka vigingi (beacons) katika eneo hilo na wanafanya kazi hiyo kwa nguvu na vitisho kwa kutumia wanajeshi wenye silaha kusimamia kazi hiyo.

RC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kupitia kwa wakili wa Serikali aliyetajwa kwa jina moja la Marco, walieleza kulikuwa hakuna amri yoyote inayoishi, inayotakiwa kubatilishwa na mahakama hiyo.

Walieleza alichofanya RC halikuwa tamko, bali ilikuwa ni kuwajulisha tu wanavijiji hao kuhusu nini Serikali inafanya katika kuthibitisha mipaka ya KIA na watakaokutwa ndani ya eneo la KIA kwa kujua au kutokujua, haki yao itazingatiwa.

RC na AG katika utetezi wao walieleza wananchi hao walijulishwa haki yao itazingatiwa kabla ya kuamriwa kuondoka katika eneo hilo na hakuna nguvu imetumiwa na wawili hao katika kuwajulisha wananchi hao.

Walieleza katika majibu yao kuwa, RC asingeweza kutangaza KIA ndiyo wamiliki kwa sababu hati ya kumiliki eneo hilo ilitolewa na Kamishna wa Ardhi mwenye dhamana.

Hukumu ya Mahakama

Jaji Kilimi katika uamuzi amesema amepakua na kusikiliza video iliyowasilishwa kortini kama kielelezo kuthibitisha kauli ya RC, lakini aliposikiliza hajaona mahali ambako RC alitoa amri ya kuwaondoa wadai katika ardhi hiyo.

Kilichomo ni kuwa RC hakufanya lolote zaidi ya kuwajulisha wananchi waliohudhuria katika mkutano wa hadharani kuwa Serikali inafanya uhakiki wa mipaka ya KIA na atakayekuwa ndani ya eneo la KIA masilahi yake yangelindwa kabla ya kuondolewa.

Jaji amesema suala la pili ni RC Kilimanjaro aliwajulisha wananchi kuwa kinachofanyika ni kuthibitisha mipaka ya KIA ambayo imepewa nguvu na haki ya umiliki iliyotolewa kwa KIA na Kamishina wa Ardhi ambaye ndiye mwenye mamlaka hayo.

Kulingana na Jaji, kilichosemwa katika mkutano huo ni kwamba, RC alikuwa anatumia mamlaka yake kama mlinzi wa amani na alikuwa ana wajibu huo wa kuwafanya wananchi wawe na ufahamu kwa jambo lolote ambalo Serikali inafanya.

“Madai ya waombaji kuwa Novemba 9, 2022 kazi ya uwekaji vigingi ilianza naona si haki kuhusiana na nani anawajibika kwa sababu uthibitisho kama waliokuwa wanaweka vigingi walitumwa na RC Kilimanjaro au Kamishina wa Ardhi,” amesema Jaji Kilimi.

Kutokana na maelezo hayo, Jaji Kilimi amesema ameridhika kuwa maombi ya wananchi hao hayakukidhi masharti ya kupewa amri ya kubatilisha agizo lililodaiwa ni la RC, hivyo linatupwa na kwa asili ya shauri hilo, kila upande utabeba gharama zake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live