Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi yawasaka watu wawili vinara wa mauaji ya visu

Vinara Visu Polisi yawasaka watu wawili vinara wa mauaji ya visu

Mon, 5 Sep 2022 Chanzo: BBC

Polisi nchini Canada wameanzisha msako mkali kuwasaka wanaume wawili wanaoshukiwa kuwachoma visu takriban watu 10 katika shambulio ambalo limeshangaza taifa.

Washukiwa wawili waliotajwa kama Damien Sanderson na Myles Sanderson wametoroka na wanadhaniwa kuwa na silaha hatari.

Wahasiriwa walipatikana katika maeneo 13 katika kijiji cha jamii ya watu wa asili huko James Smith Cree Nation karibu cha Weldon.

Ni kati ya matukio mabaya zaidi ya unyanyasaji mkubwa ambao Canada imewahi kushuhudia.

Wakati habari za kuchomwa visu zikitokea, tahadhari ya mtu hatari ilitumwa kwa simu zote za rununu katika majimbo ya Saskatchewan, Manitoba na Alberta - eneo kubwa karibu nusu ya ukubwa wa Uropa.

Wakaazi wametakiwa kuchukua tahadhari, huku msako mkali ukiendelea katika eneo kubwa la kijiografia.

‘’Usiondoke mahali salama. Tahadhari ukiruhusu wengine kuingia katika makazi yako,’’ Polisi ya jimbo la Saskatchewan imetuma ujumbe huo kwenye Twitter.

Vituo vya ukaguzi vimeanzishwa, huku polisi wakikagua vitambulisho vya wasafiri na madereva wamehimizwa kutowabughudhi wasafiri.

Hali ya hatari imetangazwa katika jimbo la James Smith Cree – eneo la watu asili lenye wakazi wapatao 2,000 kaskazini-mashariki mwa Weldon, ambapo takriban watu 200 wanaishi.

Waziri Mkuu Justin Trudeau alielezea shambulio hilo kwenye Twitter kama ‘’la kutisha na ya kuvunja moyo’’

‘’Nimeshtushwa na kuhuzunishwa na mashambulizi ya kutisha leo,’’ alisema katika taarifa tofauti.

‘’Wale waliohusika na mashambulizi ya leo ya kuchukiza lazima wafikishwe mbele ya sheria kikamilifu.’’

Katika mkutano na wanahabari Jumapili jioni, polisi walisema kunaweza kuwa na watu wengi waliojeruhiwa kuliko wale 15 ambao tayari wanajua kuwahusu, ambao walikuwa wamejipeleka hospitalini.

Rhonda Blackmore, Afisa Mkuu wa Polisi huko Saskatchewan alisema kuwa baadhi ya watu wanaweza kuwa walilengwa na washukiwa hao wawili, huku wengine wakiaminika ‘’walishambuliwa bila mpangilio’’.

Uhusiano kati ya Damien Sanderson, 31, na Myles Sanderson, 30, hauko wazi, na mamlaka hadi sasa haijatoa maelezo zaidi.

Simu ya kwanza ya dharura ilipigwa kwa polisi saa 05:40 kwa saa za huko Jumapili asubuhi katika mji mkuu wa mkoa wa Regina, karibu kilomita 280 (maili 173) kusini mwa Weldon, Bi Blackmore alisema.

Hili lilifuatiwa haraka na simu nyingi zaidi za kuomba usaidizi, na kuwa ‘’tukio linaloendelea kujitokeza kwa kasi’’.

Washukiwa hao walionekana mara ya mwisho na umma huko Regina wakati wa chakula cha mchana siku ya Jumapili, na huenda walikuwa wakisafiri kwa gari nyeusi aina ya Nissan Rogue, alisema.

‘’Wanaonekana kuwa na silaha na ni hatari... Ukiwaona washukiwa au gari lao usiwasogelee, mara moja ondoka eneo hilo na upige simu kwa polisi kupitia nambari 911.’’

Mkazi wa Weldon, Diane Shier alisema kuwa jirani yake, mwanamume aliyekuwa akiishi na mjukuu wake, aliuawa, gazeti la Globe and Mail liliripoti.

Alielezewa na mkazi mwingine, Robert Rush, kama mwanamume mpole, mjane katika miaka yake ya 70.

Ratiba ya matukio

05:40 - Saa za eneo hilo, tarehe 4 Septemba (11:40 GMT) - polisi wakapokea simu ya kwanza kuhusu shambulizi la watu kuchomwa kisu katika jimbo la James Smith Cree Nation. Simu zaidi zikaanza kuingia ndani ya dakika chache

07:12 - Polisi wakaambia umma watafute makazi salama kwengineko haraka iwezekanavyo na kutoa tahadhari ya uwepo wa watu hatari

07:57 - Polisi wakafichua majina, maelezo na picha za washukiwa hao wawili

08:20 - Tahadhari ya watu hatari ikatolewa tena katika mkoa wote wa Saskatchewan

11:25 -Msako wa kuwatafuta washukiwa hao ukajumuisha hadi mikoa jirani ya Manitoba na Alberta

12:07 -Polisi walitahadharisha umma kwamba gari la mshukiwa lilikuwa limeonekana katika eneo la Regina, mji mkuu wa mkoa

Chanzo: BBC