Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi yawanasa wanaodaiwa kutumia majina ya Jokate, Nandy kutapeli watu

Majina Pic Data Polisi yawanasa wanaodaiwa kutumia majina ya Jokate, Nandy kutapeli watu

Tue, 27 Sep 2022 Chanzo: Mwananchi

Jeshi la Polisi mkoani hapa linawashikilia watuhumiwa 23 wakiwamo wanne wanaotuhumiwa kutumia majina ya viongozi wa serikali na watu maarufu kwa utapeli na wizi wa mtandao kujiingizia kipato kwa njia isiyo halali.

Akizungumza Septemba 26, Kamanda wa Polisi mkoaniĀ  hapa, Benjamin Kuzaga amesema katika msako walioufanya kwa siku saba, wamenasa watuhumiwa hao kwa makosa mbalimbali ikiwamo wizi wa vyombo vya moto kama magari na pikipiki.

Amesema Jeshi hilo liliendesha msako mkoani humo na kubaini watuhumiwa wa uhalifu wakiwamo watu watano wanaodaiwa kuiba magari na pikipiki, wanne wakidaiwa kufanya utapeli wa mitandaoni, saba wakidaiwa kuuza wa pombe haramu na sita wakidaiwa kukutwa na dawa za kulevya.

"Hawa wanne, Ezekiel Simon, Amasha Mernad, Shaban Amidu na Benny Julius wote wakazi wa mji mdogo wa Mbalizi walitumia majina ya Jokate Mwegelo na Faustina Charles 'Nandy' kutapeli watu wakiwaahidi ajira Jeshi la Polisi na JKT, na kutuma ujumbe wa Tuma pesa kwa namba hii," amedai Kuzaga.

Kamanda huyo ameongeza kuwa watuhumiwa hao walipekuliwa kwa mujibu wa sheria na kukutwa na laini 36 za mitandao mbalimbali zenye majina na umiliki wa watu wengine, simu saba za mkononi, nyaraka mbalimbali, picha na machapisho.

Kamanda huyo ametoa rai na wito kwa wananchi wanaomiliki silaha kinyume na utaratibu kuziwasilisha mapema kwa kipindi hiki, kuanzia Septemba 1 hadi Oktoba 31 akibainisha kuwa baada ya muda huo Operesheni kabambe itapita maeneo yote na watakaobainika itatumika lugha nyingine.

Aidha, Kamanda huyo ameelezea ajali ya gari aina ya Leyland DAF iliyokuwa na mafuta ya dizeli iliyokuwa iliyotokea leo asubuhi mtaa wa Sae jijini hapa akibainisha kuwa hakuna vifo wala majeruhi na kwamba Jeshi la Polisi liliingilia mapema kuwatawanya wananchi waliokuwa wakienda kuchota mafuta ili pasitokee madhara yoyote.

"Gari hilo mali ya Coy Olympic likitokea Dar es Salaam kwenda Tunduma lilipata ajali baada ya dereva kushindwa kulimudu baada ya kupitwa na usingizi na kulisukuma huko, lakini Polisi tulifika mapema na kutawanya watu ili wasiende kuchota mafuta, hakuna vifo wala majeruhi," amesema Kamanda huyo.

Chanzo: Mwananchi