Dar es Salaam.Jeshi la polisi Dar es Salaam limewakamata walioratibu maandamano kwenda ubalozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania kushinikiza ndege ya Air Tanzania iliyozuiwa nchini humo kuachiwa.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa akizungumza baada ya kuwatawanya waandamanaji hao amesema, “Tumewakamata wale ambao wameratibu na kuongoza maandamano hayo, Chochote ambacho wanataka kupeleka kwa umma, wanaweza kuandika barua au kutuma wawakilishi.”
Amesema Serikali ya Tanzania imepeleka watu Afrika Kusini kushughulikia suala hilo, kuwataka Watanzania kuwa watulivu, wasubiri hatua zitakazochukuliwa.
“Hili ambalo wamelifanya la kuandamana halikubaliki. Tuheshimu sheria hata pale tunapoona jambo linafanyika halipendezi lakini kuheshimu sheria ni jambo la maana sana,” amesema Mambosasa.
Juzi msemaji wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbas amesema ndege hiyo imezuiwa kutokana na kesi ya madai iliyofunguliwa na Hermanus Steyn.
Steyn, raia wa Afrika Kusini anadai fidia baada ya mali zake kutaifishwa na Serikali ya Tanzania mwaka 1980.