Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi yaomba ushirikiano uchunguzi mauaji ya padri

73cf58c8dda425c47436d1f442e4c148 Polisi yaomba ushirikiano uchunguzi mauaji ya padri

Tue, 14 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limesema linaendelea na uchunguzi wa mauaji ya Padri wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya, Michel Samson (63) yaliyofanyika usiku wa kuamkia Juni 11, mwaka huu.

Ili kufanikisha uchunguzi huo, jeshi hilo limeomba ushirikiano kutoka kwa raia wema iwapo wanazo taarifa juu ya tukio husika sambamba na walipo waliohusika na mauaji hayo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Ulrich Matei aliwaambia waandishi wa habari kuwa kuwa ushirikiano wa wananchi unahitajika hivyo kwa yeyote aliye na taarifa ni muhimu akaziwasilisha kwa jeshi hilo.

Kwa mujibu wa Kamanda Matei, mwili wa padri huyo ulikutwa Juni 11, mwaka huu saa 11:00 alfajiri maeneo ya Sabasaba jijini Mbeya ukiwa chini ya Daraja la Mto Meta.

Alisema padri huyo alikutwa akiwa ameuawa na mwili wake ukiwa umetenganishwa kichwa na kiwiliwili na kisha kuviringishwa duveti na blanketi na kutupwa kwenye mto huo na watu wasiofahamika.

Alisema padri huyo raia wa Malawi alikuwa akihudumu katika Shirika la Missionaries of African (White Fathers).

Awali Juni 10 saa 11:00 jioni padri huyo aliwaaga wenzake kuwa anakwenda kufanya mazoezi ya kutembea na hakurudi tena mpaka alipokutwa ameuawa umbali wa takribani kilometa mbili kutoka maeneo ya parokiani wanapoishi na mapadri wenzake wa shirika hilo.

“Msako unaendelea ili kuwabaini na kuwakamata wote waliohusika na tukio hilo. Jeshi la Polisi linalaani vikali tukio hili baya kutokea ndani ya mkoa wetu kwa siku za hivi karibuni.

“Lakini tunatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za watu waliohusika na tukio hili kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili watuhumiwa wakamatwe na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao. Pia Jeshi la Polisi mkoani hapa linaendelea na upelelezi wa tukio hili ili kubaini chanzo chake na waliohusika kwa hatua zaidi za kisheria,” alisema Kamanda Matei.

Katibu wa Jimbo Kuu la Mbeya, Padri Daniel Sitayila jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa taarifa za utaratibu wa msiba huo zitatolewa leo na Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga atakapozungumza na wanahabari baada ya kurejea kutoka Songwe alikokuwa kikazi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live