Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi yanasa watuhumiwa 12 wizi mtandaoni

08e1a08cce1b56bfac0193bc5215e3c4 Polisi yanasa watuhumiwa 12 wizi mtandaoni

Sat, 26 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watu 12 kwa makosa ya kujishughulisha na wizi wa mtandaoni kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali.

Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Jumanne Muliro alitoa taarifa hiyo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu matukio mbalimbali ya uhalifu ikiwamo lingine la mkazi wa Chamazi Temeke, Haji Mussa (30) anayetuhumiwa kumshambulia kwa fimbo na kumsababishia maumivu makali mtoto wake wa kambo akimtuhumu kuiba fedha.

Akizungumzia watuhumiwa hao wa wizi wa mtandaoni, Muliro alisema watu hao walikamatwa kutokana na operesheni maalumu iliyofanyika kuanzia Februari 6 hadi 20 mwaka huu. Alisema watuhumiwa hao walikutwa wakiwa na kompyuta mpakato moja mali ya Kampuni ya Tigo, EFD mashine moja, simu za mkononi 42, kadi za Tigo (line) 55, nyaraka zenye kurasa 1,500 ambazo ni taarifa za mawakala wa mtandao wa Tigo nchi nzima.

Kamanda alisema watu hao pia walikutwa wakiwa na nyaraka zenye taarifa za wateja wa CRDB walivyokuwa wakivitumia kufanyia wizi kupitia kwa mawakala huku mmoja akijifanya kuwa mteja ambaye hupiga simu au kuwatumia ujumbe wakijifanya ni wafanyakazi wa kampuni ya simu za mkononi.

“Wakati mwingine wezi hao hutoa maelekezo kwa kujifanya wanahuisha mfumo wa kampuni wanaokutajia na mwisho hukuelekeza kuweka namba yako ya siri baada ya hapo mhusika hujikuta ameibiwa fedha kutoka kwenye akaunti yake,” alisema.

Aidha, Kamanda Muliro aliwataka watu wote walioibiwa kwa njia ya mfumo huo wafike Kituo cha Polisi Oysterbay mahali ambako upelelezi wa watu hao unaendelea taratibu za kisheria zikamilishwe na baadaye watuhumiwa hao waweze kufikishwa mahakamani.

Katika tukio la baba aliyemshambulia mtoto wa kambo, kamanda alimtaja mtoto huyo, Feisali Deogratia Masawe (11) kuwa ni mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Chamazi Dovya. Kwa mujibu wa Muliro, baba huyo alimpa adhabu mtoto huyo akimtuhumu kuwa amemuibia Sh 195,000 usiku wa Februari 22 mwaka huu.

Tukio lilibainika Februari 23 baada ya mtoto huyo kudondoka na kupoteza fahamu akiwa maeneo ya shuleni.

Alisema baadaye mtoto huyo alipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na baada ya kufanyiwa uchunguzi wa awali ilibainika kuwa chanzo cha kudondoka kwake ni kipigo alichokipata kutoka kwa baba yake wa kambo.

“Kitendo kilichofanywa na mtuhumiwa ni ukatili uliopita kiasi na jeshi haliwezi kuvumilia vitendo kama hivyo na kwa sababu hiyo mtuhumiwa atafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo kujibu tuhuma zinazomkabili,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live