Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi yampa dhamana UVCCM anayetuhumiwa kumtukana Magufuli

61530 UVCCM+PIC

Thu, 6 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kijana wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi(UVCCM), Mussa Badi aliyekamatwa wiki chache zilizopita akidaiwa kumtukana Rais John Magufuli ameachiwa kwa dhamana katika Kituo cha Msimbazi, Jijini Dar es Salaam huku mapya yakiibuka. 

Taarifa za kukamatwa kwa Badi zilianza kusambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii kwa baadhi ya watu kusema alikamatwa na polisi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa leo Alhamisi ya Juni 6, 2019 ameliambia Mwananchi kuwa kijana huyo alikamatwa na Jeshi la Polisi kwa madai ya kumtukana Rais Magufuli lakini kwa sasa ameachiwa kwa dhamana na uchunguzi wa tuhuma zake bado unaendelea.

“Ni kweli alikamatwa kwa madai ya kutoa maneno ya kashfa, lakini waliolalamika ni wenzake, sisi  kazi yetu tulimkamata na kuanza kuchunguza, uchunguzi bado haujabaini kilichokuwa kinalalamikiwa kwa hiyo bado tunaendelea kufuatilia ndiyo maana ameachiwa kwa dhamana wakati tukiendelea na uchunguzi,” amesema Mambosasa.

Alipoulizwa muhusika wa malalamiko hayo dhidi ya Badi, Mambosasa alisema: “Nikisema mlalamikaji alitoka eneo hilo maana yake ni watu wa chama wenyewe.”

Kamanda Mambosasa alipoulizwa pengine hatua ya kukamatwa kwake kulikuwa na uhusiano na uchaguzi huo wa NEC, Mambosasa alisema hajui. “Mimi sijui, mtu anapokuja kulalamika utaanza kumuuliza unalalamika.hayo maswali ni ya kuwauliza wenyewe kule(CCM).”

Pia Soma

Mwananchi limedokezwa na baadhi ya watu na viongozi wa chama hicho kuwa Badi alitengenezwa kashfa hiyo ili kumwondoa katika mbio za kugombea nafasi moja ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kupitia UVCCM.

Moja ya vyanzo kutoka UVCCM vinasema umoja huo hutoa uwakilishi wa vijana watano (watatu bara na wawili Zanzibar) watakaokuwa wajumbe wa NEC.

“Lakini uchaguzi huo ulikuwa unaziba nafasi ya mjumbe mmoja aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya, nadhani ni DC wa Namtumbo mkoani Ruvuma Sophia Kizigo, kwa hiyo uchaguzi ulifanyika na waliogombania nafasi ni watatu lakini alishinda Jafari Mughamba,” kilieleza chanzo hicho.

Naye Bakari Said ambaye ni kada wa chama hicho na rafiki wa karibu wa Badi amesema katika tukio hilo lililotokea zaidi ya wiki tatu zilizopita katika ofisi za chama za Lumumba wakati wa mkutano wa umoja huo, Badi alikamatwa na askari wa chama maarufu Green guard. 

“UVCCM huwa wanajichagua wenyewe lakini kwa sababu alikuwa na uwezo mkubwa, alikuwa na ushawishi ikabidi wamtengenezee tuhuma na alikamatwa na green guard wa chama na kuondolewa jengo la CCM, amefikishwa Polisi ikabidi wamuhifadhi tu bila kosa lolote hadi uchaguzi ulipomalizika, kwa sasa amerudi mtaani hapa hayo vizuri kisaikolojia,” amesema Bakari.

Mwananchi limemtafuta Badi kwa simu licha ya kukiri kukutana na changamoto hiyo ya hujuma ya uchaguzi amesema suala hilo lingehitaji mazungumzo ya kina na kumtaka mwandishi kwenda kukutana nae Magomeni jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, mwandishi alipofika Magomeni ambapo alimwelekeza atakuwa, simu yake haikuwa haikupatikana.

Katibu Mkuu wa UVCCM, Raymond Mwangwala ameahidi kutoa ufafanuzi wa sakata hilo hapo baadaye baada ya kudai yuko msibani kwa sasa.Katibu wa siasa na uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Simon Mwakifamba alisema kwa kuwa tukio hilo lilitokea katika ofisi za Chama Taifa, asingependa kulitolea ufafanuzi na hajafanikiwa kukaa na Badi kuzungumzia suala hilo baada ya kutoka kwa dhamana.

“Hizo taarifa sizifahamu na sijakaa naye (Badi) lakini hata hivyo mimi siyo msemaji kwa namna jambo hilo lilikuwa kwenye level(ngazi) ya Taifa, siyo ngazi ya mkoa. Inasemekana yeye alikamatiwa ofisi za makao makuu ya chama pale kwa hiyo siyo jambo lenye level yetu,” amesema Mwakifamba.

Chanzo: mwananchi.co.tz